Mazungumzo ya Vienna, maendeleo na changamoto zake
Katika fremu ya utekelezaji wa hatua za kistratijia kwa ajili ya kufuta vikwazo vya kidhalimu na kulinda maslahi ya taifa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilichukua hatua za kulipiza kisasi ikijibu hatua ya Marekani na kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na vilevile hatua ya nchi za Ulaya ya kutotekeleza majukumu yao kwa mujibu wa makubaliano hayo.
Sambamba na hayo, lengo kuu la Iran ni kulindwa makubaliano hayo kama waraka wa kujenga hali ya kuaminiana. Kwa msingi huo, hivi sasa kunafanyika kikao cha Kkamisheni ya Pamoja ya JCPOA katika ngazi ya wakurugenzi na manaibu mawaziri wa mambo ya nje wa Iran na nchi wanachama katika kundi la 4+1 huko Vienna nchini Austria. Ratiba na malengo ya mazungumzo hayo ya Vienna viko wazi. Vikwazo vyote vya Marekani vinapaswa kuondolewa, na baada ya kujihakikishia kwamba suala hilo limefanyika, Iran itasitisha hatua zake za kulipiza kisasi na kutekeleza tena vipengee vyote vya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Jumanne ya jana baada ya kumalizika kikao cha Kamisheni ya Pamoja ya JCPOA, Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran Sayyid Abbas Araqchi alisema kuwa, vikwazo vyote vilivyowekwa na Marekani baada ya kusainiwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, sawa viwe vimewekwa katika kipindi cha utawala wa Barack Obama au kipindi cha utawala wa Donald Trump vinapaswa kuondolewa. Araqchi amesema kumepatikana maendeleo katika makundi mawili ya mazungumzo hayo yanayojadili masuala ya nyuklia na kuondolewa vikwazo na kuongeza kuwa, makundi hayo sasa yanatayarisha muswada wa maapatano.
Hata hivyo Sayyid Abbas Araqchi ametilia mkazo umuhimu wa masuala yanayojadiliwa hii leo katika kundi la tatu la Kamisheni ya Pamoja ya JCPOA huko vienna na kusema kuwa: Kazi ya kundi hilo ni kijadili jinsi ya kudhamini na kupata hakikisho la kuondolewa vikwazo, muda wake na kuainisha kipindi maalumu cha kila upande kuwa umetekeza majukumu yake kwa mujibu wa makubaliano hayo ya nyuklia.
Kutokana na matamshi hayo ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, tunaweza kusema kuwa, mazungumzo ya Vienna yamepiga hatua nzuri. Hata hivyo hayapaswi kurefushwa kupita kiasi, kwani uzoefu wa huko nyuma umeonyesha kuwa, "mazungumzo kwa ajili ya mazungumzo tu" hayawezi kusaidia juhudi za kutatua matatizo yanayohusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Wakati huo huo balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika taasisi za kimataifa mjini Vienna alisema wiki iliyopita kwamba: Msingi wa timu ya mazungumzo ya Iran ni mambo yaliyoainishwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu kadhia hii kama sera kuu za utawala wa Kiislamu.
Ukweli ni kuwa, msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA uko wazi; kwa msingi huo suala la kuhuishwa makubaliano hayo haliwezi kutimia bila ya kuondolewa vikwazo vyote vya Marekani dhidi ya Iran. Kufutwa vikwazo karibu 1,600 vilivyowekwa dhidi ya Iran itakua hatua muhimu inayopaswa kuchukuliwa na Marekani katika uwanja huu.
Naibu Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya, Enrique Mora anasema kuwa, ufunguo na siri ya mafanikio ya mazungumzo ya sasa ni kwamba, pande zote zinaitaka Marekani irejee katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kutekeleza vipengee vyake.
Kwa kutilia maanani haya yote na historia ya huko nyuma, ni vigumu kutoa tathmini kamili kuhusiana na matokeo ya mazungumzo ya sasa huko Vienna. Hapana shaka kuwa mazungumzo hayo yatafanikiwa pale pande zote zitakapokuwa na irada na azma madhubuti, na kurejesha tena hali ya kuaminiana iliyoharibiwa na washirika wa Magharibi katika makubaliano ya JCPOA.