Hatua mpya za vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran
Wizara ya Biashara ya Marekani Alkhamisi ya jana iliwaweka watu na mashirika kadhaa katika orodha yake ya vikwazo kwa kisingizio cha nafasi yao katika kudhamini fedha kwa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah) na harakati ya wapiganaji wa kujitolea ya Ansarullah nchini Yemen.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Fedha ya Marekani imesema kuwa, imeuwekea vikwazo mtandao unaosadia kudhamini fedha kwa ajili ya Kikosi cha Quds na wapiganaji wa Ansarullah wa Yemen. Wizara hiyo imeyaweka kwenye orodha ya vikwazo majina ya watu 7 na mashirika 4 kwa kutumia agizo la utekelezaji nambari 13224. Kikosi cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran (Sepah) pia kiliwekwa kwenye oroda hiyo hapo mwaka 2007 kwa kutegemea agizo hilo hilo.
Katika upande mwingine, Wizara ya Fedha ya Marekani imechukua hatua tofauti na kutangaza kwamba, imewaondoa maafisa watatu za zamani wa serikali ya Iran katika orodha yake ya vikwazo. Wizara hiyo pia imeyandoa majina ya mashirika matatu kwenye orodha hiyo ambayo awali yaliwekewa vikwazo kwa tuhuma za kufanya biashara, kuuza na kusafirisha au kutafuta soko kwa ajili ya bidhaa za petrokemikali za Iran. Taarifa ya Wizara ya Biashara ya Marekani imedai kuwa, hatua hiyo imechukuliwa kama matokeo ya kubadilika mienendo au hali ya watu na taasisi hizo. Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani, Ned Price amesema, hakuna mfungamano wa aina yoyote baina ya kuondolewa kenye orodha ya vikwazo maafisa hao 3 wa zamani wa Iran na mazungumzo yanayoendelea sasa huko Vienna kwa ajili ya kuokoa mapatano ya nyuklia ya JCPOA.
Inaonekana kuwa, kwa hatua hii, yaani kuweka vikwazo vipya na kufuta baadhi ya vikwazo vya zamani dhidi ya maafisa au taasisi zenye ushirikiano na Iran, serikali ya Joe Biden inataka kuonesha kuwa, japokuwa bado inaendeleza sera za kuiwekea vikwazo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na washirika wake wa kikanda, lakini wakati mwingine inaweza kufuta baadhi ya vikwazo hivyo kwa kile inachodai ni kuonyesha "nia nje". Hata hivyo inatupasa kuashiria masuala kadhaa uhusiana na madai haya:
Kwanza ni kuwa, sera mpya za vikwazo za serikali ya Joe Biden dhidi ya Iran tunaweza kuzifupisha katika maneno machache ambayo ni, "ondoa majina kadhaa katika orodha ya vikwazo dhidi ya Iran na wakati huo huo weka majina mengi zaidi kwenye orodha hiyo". Kwa maneno mengine ni kuwa, ili kuzihadaa fikra za walimwengu kwamba ina nia ya kufikia mapatano na Iran, Washington imechukua hatua ya kuyafuta baadhi ya majina ya maafisa wa zamani wa Iran na washirika wake katika orodha ya vikwazo ya Wizara ya Biashara ya Marekani baada ya kuthibtika kwamba kuwawekea vikwazo hakuna tena maana yoyote kwa sababu moja au nyingine. Ukweli ni kwamba serikali ya Washington inafuatilia malengo yaleyale ya siasa zake katika eneo la Mashariki ya Kati kwa kuzidisha mashinikizo dhidi ya Tehran na washirika wake kupitia njia ya vikwazo vya aina mbalimbali.
Nukta ya pili ni kwamba, vikwazo hivi vipya vya serikali ya Biden vinaonyesha kuwa, licha ya madai ya Washington ya eti kutupilia mbali sera za serikali ya Trump kuhusiana na Iran katika fremu ya "mashinikio ya kiwango cha juu zaidi" kwa kuiwekea Tehran vikwazo ambavyo havijawahi kushudiwa katika historia, lakini ukweli ni kwamba, tangu iliposhika madaraka, serikali ya Joe Biden imedumisha mashinikizo na vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu kwa njia mbalimbali. Si hayo tu, bali hata katika mazungumzo yanayoendelea sasa huko Vienna kwa ajili ya kuhuisha makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Marekani haiko tayari kulegeza hata kidogo msimamo wake katika uwanja huo.
Tatu ni kwamba, serikali ya Biden imesema mara kwa mara kwamba itachunguza suala la kufuta vikwazo vinavyopingana na makubaliano ya JCPOA tu; hivyo hakuna uwezekano wa kufutwa vikwazo vingine vilivyowekwa na serikali ya Trump kwa kutumia visingizio vingine kama madai kwamba, Iran inaunga mkono ugaidi. Hii ni licha ya kwamba, Jamhuri ya Kiislamu inataka kufutwa vikwazo vyote 1500 ilivyowekewa na Marekani katika kipindi cha utawala wa Donald Trump.
Kwa kuzingatia hayo yote tunaweza kusema kuwa, sera ya serikali ya Joe Biden inaendeleza siasa zilezile zilizofeli na kushindwa za serikali ya Donald Trump dhidi ya Iran.