Jun 20, 2021 02:22 UTC

Rais mteule wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliyeshinda katika uchaguzi wa 13 wa rais uliofanyika juzi Ijumaa humu nchini amesema kuwa, serikali atakayounda itafanya juhudi zake zote kutatua matatizo yaliyopo nchini hasa ya kiuchumi.

Shirika la habari la Iran Press limemnukuu Sayyid Ebrahim Raisi akisema hayo jana mbele ya waandishi wa habari na kusema: "Bila ya shaka yoyote nitashirikiana vilivyo na Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran), wabunge na kamati zao pamoja na watu muhimu na wanafikra mbalimbali katika kuunda serikali ambayo itafanya kazi kubwa ya kutatua matatizo yaliyopo nchini. Amesema nina imani serikali nitakayounda itaongeza matumaini ya mustakbali mwema kwa wananchi na imani yao kwa serikali itaongezeka siku baada ya siku.

Sayyid Raisi vile vile amesema, ninawashukuru wananchi wote azizi, wagombea wapendwa, lakini hasa hasa Kiognozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa kuandaa mazingira mazuri ya kujitokeza mamilioni kwa mamilioni ya wananchi katika uchaguzi wa 13 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Sayyid Ebrahim Raisi, mshindi wa uchaguzi wa 13 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameahidi kufanya juhudi zake zote kulitumikia vilivyo taifa

 

Aidha ameelezea matumaini yake kwamba kujitokeza mamilioni ya wananchi wa Iran katika uchaguzi wa 13 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu kutaipa nguvu serikali yake na kuisaidia sana katika kutatua matatizo hasa ya kimaisha na kuliletea taifa mustakbali bora. 

Zaidi ya Wairani milioni 59 walikuwa wametimiza masharti ya kupiga kura katika uchaguzi ambao ulikuwa wa wagombea wanne baada ya Wagombea wengine watatu kujiondoa katika mchuano huo Jumatano.

Juzi Ijumaa pia kulifanyika uchaguzi wa mabaraza ya Kiislamu ya miji na vijiji na halikadhalika uchaguzi mdogo wa bunge na baraza la wataalamu wanaomchagua Kiongozi Muadhamu.

Tags