Jun 19, 2021 14:13 UTC
  • Matokeo rasmi ya uchaguzi wa rais wa Iran yatangazwa

Baada ya kumalizika zoezi la kuhesabu kura za uchaguzi wa 13 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iran imetangaza matokeo rasmi ya uchaguzi huo ulioshirikisha mamilioni ya wapiga kura.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran Press, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abdolreza Rahmani Fazli ametangaza matokeo hayo leo Jumamosi mbele ya waandishi wa habari hapa jijini Tehran na kusema kuwa, wapiga kura milioni 28 na laki tisa na 36 elfu na nne wameshiriki katika uchaguzi wa 13 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Amesema, asilimia 48.8  ya watu waliotimiza masharti ya kupiga kura wameshiriki kwenye uchaguzi huo. Ameongeza kuwa, Sayyid Ebrahem Raeisi ndiye aliyechaguliwa kuwa Rais mpya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kura milioni 17 na laki 9 na 25,345 za wananchi.

Sayyid Ebrahim Raeisi; Rais mteule wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

 

Waziri huyo wa Mambo ya Ndani wa Iran pia amesema, Mohsen Rezaei amepata kura milioni 3 na laki nne na 12,712, Abdel Naser Hemmati amepata kura milioni 2 na laki nne na 27,201 na Sayyid Amir Hossein Qazizadeh Hasheimi amepata kura laki 9 na 99,718.

Uchaguzi wa 13 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na uchaguzi wa sita wa mabaraza ya Kiislamu ya miji na vijiji ulifanyika jana Ijumaa tarehe 18 Juni, 2021. Hiyo hiyo jana kulifanyika pia uchaguzi wa kwanza mdogo wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Kiislamu na uchaguzi wa pili mdogo wa Baraza la Tano la Wanachuoni Wataalamu wanaomchagua na kusimamia kazi za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Tags