Rais Rouhani: Kiongozi Muadhamu amewapa motisha wanasayansi kwa kupigwa chanjo ya Iran
(last modified Sat, 26 Jun 2021 12:48:05 GMT )
Jun 26, 2021 12:48 UTC
  • Rais Hassan Rouhani
    Rais Hassan Rouhani

Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema hatua ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya kupigwa chanjo ya Corona ya COVIran Barekat imewapa motisha na kuwashajiisha wanasayansi wa Jamhuri ya Kiislamu walioizalisha chanjo yenyewe.

Dakta Rouhani amesema hayo leo Jumamosi katika Makao Makuu ya Kitaifa ya Kupambana na Janga la Corona hapa Tehran na kuongeza kuwa, "taifa linapaswa kuwa na fahari kwa chanjo hii iliyozalishwa na Wairani." 

Mapema jana, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alidungwa dozi ya kwanza kabisa ya chanjo ya Corona ya COVIran Barekat na kusema kuwa: Kuna ulazima wa kuthamini na kuenzi fahari hii ya taifa ya kuzalisha chanjo ya Kiirani ya Corona.

Ayatullah Khamenei aliwashukuru wanasayansi wote vijana, wachapakazi na waliofanya bidii kubwa katika uzalishaji wa chanjo hiyo ya corona na vituo vingine vinavyofanya kazi kutengeneza chanjo nyingine hapa nchini.

Kuzinduliwa chanjo hiyo kunaiweka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika orodha ya nchi sita tu duniani zinazotengeneza chanjo ya Corona.  

Kiiongozi Muadhamu akipokea dozi ya kwanza ya Corona iliyozalishwa humu nchini

Kwengineko katika hotuba yake, Rais Hassan Rouhani amesema licha ya kuwa Iran inazalisha chanjo za ndani ya nchi, lakini kwa sasa inahitaji chanjo kutoka nje ya nchi; na kwamba baada ya miezi michache ijayo, Jamhuri ya Kiislamu haitahitajika tena kuagiza chanjo hizo kutoka nje ya nchi.

Ameeleza bayana kuwa, baada ya kutosheleza mahitaji ya ndani ya nchi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran baadaye itaanza kuuza nje ya nchi chanjo zilizozalishwa humu nchini.