Qalibaf: Vita vya 'Upanga wa Quds' viliwapa izza Waislamu
(last modified Sat, 07 Aug 2021 01:07:24 GMT )
Aug 07, 2021 01:07 UTC
  • Qalibaf: Vita vya 'Upanga wa Quds' viliwapa izza Waislamu

Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema vita vya siku 12 vya 'Upanga wa Quds' huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu viliwapa izza na kuwapandisha hadhi Waislamu kote duniani.

Muhammad Baqir Qalibaf, Spika wa Bunge la Iran amesema hayo katika mazungumzo yake hapa jijini Tehran na  Ismail Hania, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas). 

Amesisitiza kuwa, taifa la Iran litaendelea kuunga mkono muqawama wa Palestina, hadi pale taifa hilo litakapojikomboa toka kwenye makucha ya utawala ghasibu wa Israel.

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ameongeza kuwa, kitendo cha baadhi ya madola kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel kamwe hakitazima irada ya Wapalestina ya kupigania ukombozi wa nchi yao.

Amebanisha kuwa, Wazayuni hawataki kitu kingine ghairi ya kuibua mgawanyiko katika nchi za Kiislamu, lakini muqawama wa wananchi wa Palestina umekuwa na nafasi muhimu katika kusambaratisha njama hizo. 

Wanamuqawama na silaha zao

Kwa upande wake,  Ismail Hania, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) sambamba na kulishukuru taifa la Iran kwa uungaji mkono wake wa hali na mali, amesema vita vya 'Upanga wa Quds' vimeonyesha wazi kuwa, njia pekee ya kuhakikisha kuwa haki za Wapalestina na umma wa Kiislamu zinalindwa, ni kufuata njia ya muqawama na mapambano. 

Vita hivyo vya siku 12 vilianzishwa na Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan na Gaza kuanzia tarehe 10 Mei mwaka huu na kumalizika tarehe 21 mwezi huo huo baada ya utawala wa Kizayuni kuomba kusitisha mapigano baada ya kupokea kipigo kutoka kwa wanamapambano wa Palestina. 

Tags