Sep 01, 2021 07:41 UTC

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu itashirikiana na majirani zake ili kufikia upeo wa juu wa ushirikiano wa kieneo.

Hussein Amir-Abdollahian amesema hayo katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter leo Jumatano na kusisitiza kuwa: "Kushirikiana na majirani zetu ndicho kipaumbele cha kwanza cha serikali mpya ya Iran."

Ameashiria mkutano wake na Waziri Mkuu wa Imarati hivi karibuni na kueleza kuwa: Pambizoni mwa Mkutano wa Ushirikiano wa Baghdad, nilifanya mazungumzo ya kufana na Mohammed bin Rashid Al Maktoum, Waziri Mkuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu.

Abdollahian amesema: Iran na UAE zinaweza kupiga hatua kubwa kuelekea katika ushirikiano imara kwa misingi ya sera za ujirani mwema na diplomasia.

Amir-Abdollahian katika mkutano wa Baghdad

Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika mazungumzo yao hayo, waligusia juu ya azma chanya ya viongozi wa nchi mbili hizi kuimarisha ushirikiano na uhusiano wa kidugu wa mataifa mawili.

Kadhalika Hussein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Iran amesisitizia umuhimu na udharura wa kuweko ushirikiano wa kisiasa na kiusalama wa kieneo.

 

Tags