Newsweek: Uanachama wa Iran katika Jumuiya ya Shanghai umeibana Magharibi
(last modified Thu, 30 Sep 2021 06:28:10 GMT )
Sep 30, 2021 06:28 UTC
  • Newsweek: Uanachama wa Iran katika Jumuiya ya Shanghai umeibana Magharibi

Jarida la kila wiki la Newsweek la nchini Marekani limeandika kuwa, uanachama wa kudumu wa Iran katika Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai utazidi kuibana Magharibi katika kukabiliana na mradi wa nyuklia wa Iran.

Jarida hilo limeongeza kuwa, uanachama wa Iran katika Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai utasababisha matatizo makubwa ya kiistratijia kwa nchi za Magharibi katika kukabiliana na mradi wa nyuklia wa Iran.

Tarehe 17 mwezi huu wa Septemba na katika maadhimisho ya mwaka wa 26 wa kuasisiwa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai sherehe ambazo zilifanyika huko Dushanbe, mji mkuu wa Tajikistan, jumuiya hiyo iliipokea rasmi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa mwanachama wake rasmi na hayo yanahesabiwa kuwa ni mafanikio makubwa kwa Tehran.

Sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mwanachama kamili wa Jumuiya ya Ushirikiano  wa Kiuchumi ya Shanghai

 

Kuhusu mafanikio hayo, Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema kuwa, uanachama wa kudumu Iran katika Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai ni harakati ya kiistratijia na mafanikio ya kidiplomasia kwa Jamhuri ya Kiislamu.

Alisema, uanachama kamili Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika jumuiya hiyo ya Shanghai unawafanya wananchi wa Iran wawe na njia madhubuti ya mawasiliano ya kiuchumi, kwa maana ya Tehran kupata kiunganishi cha kuifikia miundombinu ya kiuchumi ya Asia na maliasili zake endelevu zinazotokana na miundombinu hiyo.

Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai iliasisiwa tarehe 15 Juni, 2001. Wakati huo wanachama wa jumuiya hiyo ya kikanda zilikuwa ni nchi za China, Russia, Kazakhstan, Kyrgyzstan, Tajikistan na Uzbekistan. Jumuiya hiyo iliundwa katika mji wa Shanghai, nchini China.

Tags