Iran yalaani vikwazo vipya ilivyowekewa na Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i76338-iran_yalaani_vikwazo_vipya_ilivyowekewa_na_marekani
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani vikwazo vipya vilivyowekwa na Marekani na akasema mashinikizo na vikwazo hivyo havitateteresha hata chembe azma ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kulinda amani na usalama wa watu wake.
(last modified 2026-05-05T14:43:53+00:00 )
Oct 30, 2021 04:35 UTC
  • Iran yalaani vikwazo vipya ilivyowekewa na Marekani

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani vikwazo vipya vilivyowekwa na Marekani na akasema mashinikizo na vikwazo hivyo havitateteresha hata chembe azma ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kulinda amani na usalama wa watu wake.

Saeed Khatibzadeh ametoa kauli hiyo kufuatia hatua ya karibuni iliyochukuliwa na wizara ya fedha ya Marekani ya kuwawekea vikwazo shakhsia binafsi na wa kisheria wa Iran, ambapo mbali na kupinga hatua hiyo amesema, uwekaji vikwazo vipya unaashiria mwenendo wenye mgongano wa waziwazi wa serikali ya Washington.

Khatibzadeh ameongeza kuwa, serikali inayosema kuwa inataka kurudi kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA huku ikiwa inaendelea kufuata njia ileile ya Trump ya kuendeleza vikwazo, inafikisha ujumbe wa wazi wa kuonyesha kwamba si ya kuaminika.


 

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa, serikali tofauti ambazo zimekuweko madarakani nchini Marekani zimeonyesha ni kwa kiwango gani zimeshindwa kuwa na uwezo wa kutambua ukweli na hali ya halisi kuhusiana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Wizara ya Fedha ya Marekani, na sambamba na kukaribia kuanza tena mazungumzo ya nyuklia ya JCPOA mjini Vienna, imewawekea vikwazo watu wanne na mashirika mawili yaliyoko katika miji ya Esfahan na Qom kwa madai kwamba yanasaidia shughuli za Iran za uundaji ndege zisizo na rubani na kuhatarisha maslahi ya Marekani.../