Iran: Marekani iwajibishwe kwa matatizo yanaoikumba Afghanistan
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Marekani na waitifaki wake wanapaswa kubebeshwa dhima kutokana na migogoro na matatizo mengine yanayoshuhudiwa hii leo nchini Afghanistan.
Ali Shamkhani amesema hayo leo katika ufunguzi wa Duru ya Tatu ya Mazungumzo ya Usalama wa Eneo ya Delhi juu ya Afghanistan na kueleza kuwa, uwajibikaji wa kiwango cha chini kabisa ni kufidia hasara zote walizowasababishia wananchi wa Afghanistan.
Ameeleza bayana kuwa, "miaka 20 iliyopita, Marekani iliikalia kwa mabavu Afghanistan kwa kisingizio cha vita dhidi ya Taliban na al-Qaeda, ikidai kuwa inapambana na ugaidi, na kudai kuwa inataka kuigeuza Afghanistan kuwa kiigizo chema na chimbuko la ilhamu."
Shamkhani amebainisha kuwa, badala ya Marekani kutekeleza iliyoyadai, imeifanya hali ya nchi hiyo kuwa mbaya zaidi, na hivi sasa vitendo vya ugaidi, umaskini na uchochole umeongezeka mno nchini Afghanistan.
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ameongeza kuwa, Marekani ilifeli hata katika mambo ya msingi kama kuimarisha mifumo ya kijeshi na usalama ya Afghanistan, na baada ya kukimbia nchini humo pamoja na waitifaki, kundi la Taliban likatwaa mamlaka ya nchi.
Marekani licha ya kutumia zaidi ya dola trilioni 2.26 kwa mujibu wa uchunguzi wa 'Mradi wa Gharama za Vita' uliofanywa na Chuo Kikuu cha Brown tokea mwaka 2001, lakini hatimaye ililazimika kuondoka kwa madhila nchini Afghanistan.