Araqchi: Marekani inabeba dhima kwa hali ya sasa Afghanistan
Katibu wa Baraza la Kistratajia la Mahusiano ya Kigeni la Iran amesema Marekani ndiyo inayopaswa kulaumiwa na kuwabishwa kutokana na matatizo mengi yanaoikumba Afghanistan.
Sayyid Abbas Araqchi alisema hayo jana katika mkutano wake na Mette Knudsen, Naibu Mwakilishi Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Afghanistan na kuongeza kuwa, Marekani na waitifaki wake wanapaswa kubebeshwa dhima kutokana na migogoro na matatizo mengine yanayoshuhudiwa hii leo nchini Afghanistan.
Araqchi ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya kisiasa katika serikali iliyopita ya Dakta Hassan Rouhani amebainisha kuwa, katika hali ambayo Jamhuri ya Kiislamu ni mwenyeji wa wakimbizi zaidi ya milioni nne wa Kiafghani, lakini mashirika ya kimataifa yamekataa kabisa kulisaidia taifa hili kuubebea mzigo wa kushughulikia maslahi ya wakimbizi hao.
Mwanadiplomasia huyo wa wa ngazi ya juu wa Iran ameeleza bayana kuwa, uwepo wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi umewasababishia matatizo chungu nzima wakazi wa eneo hili la kistratajia.
Kwa upande wake, Naibu Mwakilishi Maalumu wa UN katika masuala ya Afghanistan amesema hali inayoshuhudiwa nchini Afghanistan ni ya kutamausha, huku akiitaka jamii ya kimataifa kuzishughulikia kwa umakinifu mkubwa changamoto zinazowakabili Waafghani, haswa katika kipindi hiki cha kukaribia msimu wa baridi kali.
Marekani, licha ya kutumia zaidi ya dola trilioni 2.26 kwa mujibu wa uchunguzi wa 'Mradi wa Gharama za Vita' uliofanywa na Chuo Kikuu cha Brown cha US tokea mwaka 2001, lakini hatimaye ililazimika kuondoka kwa madhila nchini Afghanistan.