Abdollahian asisitiza msimamo wa Iran wa kuliunga mkono taifa la Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i78232-abdollahian_asisitiza_msimamo_wa_iran_wa_kuliunga_mkono_taifa_la_palestina
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, Iran itaendelea kuwaunga mkono wananchi wa Palestina hadi pale mji mtakatifu wa Quds utakapombolewa na kuondoka katika makucha ya Wazayuni maghasibu.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Dec 20, 2021 01:16 UTC
  • Abdollahian asisitiza msimamo wa Iran wa kuliunga mkono taifa la Palestina

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, Iran itaendelea kuwaunga mkono wananchi wa Palestina hadi pale mji mtakatifu wa Quds utakapombolewa na kuondoka katika makucha ya Wazayuni maghasibu.

Hussein Amir-Abdollahian amesema hayo mjini Islamabad pambizoni mwa mkutano wa Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) katika mazungumzo yake na Riyadh al-Maliki, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Palestina.

Sambamba na kusisitiza himaya na uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa wananchi wa Palestina, Hussein Amir-Abdollahian amelaani vikali jinai za utawala haramu wa Kizayuni wa Israel katika ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu.

Wakati huo huo, akizungumza jana katika kikao cha dharura cha Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kilichofanyika mjini Islamabad, kwa ajili ya kujadili matukio ya Afghanistan, Amir-Abdollahian alisema kuwa, amani endelevu na ya kudumu itaweza kupatikana tu nchini Afghanistan ikiwa itaundwa serikali shirikishi na itakayojumuisha pande zote.

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC)

 

Aidha alisema kuwa, kucheleweshwa kwa jambo hilo kutawapa fursa maadui wa Afghanistan ili sambamba na kushamirisha ugaidi wa Kidaesh, wawazidishie matatizo ya kiuchumi na hali mbaya ya maisha na ya kiafya watu wa nchi hiyo, kuwafanya washindwe kujikimu kwa mahitaji yao ya msingi ya maisha, kuustawisha upya mtandao mpana wa uhalifu wa kijamii na kuzidisha umasikini na baa la njaa baada ya miaka 20 ya nchi hiyo kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu na kuteketezwa miundomsingi yake yiote na hivyo kuwafanya viongozi na watu wake washindwe kufanya chochote.