Amir-Abdollahian asisitiza kuondoka askari wa Marekani katika ardhi ya Iraq
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza katika kikao cha pamoja na waandishi wa habari akiwa na mgeni wake Fuad Hussein, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iraq hapa mjini Tehran juu ya udharura wa kuondoka kikamilifu askari wa Marekani katika ardhi ya Iraq.
Hussein Amir-Abdollahian amesema: Tukiwa tunakaribia kuingia katika mwaka wa pili wa kumbukumbu ya kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qasem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Kiislamu (SEPAH) na Abu Mahdi al-Muhandis, aliyekuwa Naibu wa Mkuu wa Kikosi cha Kujitolea cha Wananchi wa Iraq al Hashd al Shaabi, tumesikia habari njema kutoka Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iraq za kuondoka wanajeshi wa Marekani kutoka katika nchi hiyo.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema kuwa, katika mazungumzo yake na Fuad Hussein, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iraq kumetiliwa mkazo suala la kuharakishwa kazi ya ufuatialiaji ya kamati ya pamoja ya kimahakama ya pande mbili kuhusiana na faili la mauaji ya Luteni Jenerali Qasem Soleimani.
Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH, Abu Mahdi al Muhandis, Naibu wa Mkuu wa Kikosi cha Kujitolea cha Wananchi wa Iraq al Hashd al Shaabi pamoja na wenzao wengine wanane waliuliwa shahidi usiku wa kuamika Ijumaa tarehe tatu Januari 2020 katika shambulio la anga lililofanywa na utawala wa kigaidi wa Marekani karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad, mji mkuu wa Iraq.