Balozi za Iran na Saudia kufunguliwa tena karibuni
Mwanachama wa Kamati ya Usalama wa Taifa na Sera za Kigeni ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu na Saudia upo katika mkondo wa kuhuishwa.
Mbunge huyo wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Jalil Rahimi Jahan-Abadi amesema hayo katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter mapema leo Jumamosi na kuongeza kuwa, nchi mbili hizi zinajiandaa kufungua balozi zao katika nchi hizo.
Amesema kufunguliwa balozi za nchi mbili hizi kutakuwa na taathira chanya; kwanza, katika kupunguza taharuki katika eneo, na pili, kuimarisha mshikamano na utangamano katika ulimwengu wa Kiislamu.
Katika miezi michache iliyopita, kumefanyika mawasiliano ya mara kwa mara kati ya Iran na Saudi Arabia, na mazungumzo mazuri yamefanyika juu ya maswala yanayozihusu pande mbili.
Akizungumzia hali ya hivi karibuni ya mazungumzo ya Iran na Saudia, Saeed Khatibzadeh, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alisema kuwa, kumekuwepo mazungumzo kadhaa baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na serikali ya Saudi Arabia huko Baghdad na kuongeza kuwa, kuna maendeleo ya kuridhisha katika mazungumzo yanayohusiana na usalama wa Ghuba ya Uajemi.
Mwishoni mwa mwaka uliopita, uhusiano wa kiuchumi wa Iran na Saudi Arabia ulianza rasmi baada ya meli moja yenye bidhaa za Jamhuri ya Kiislamu kutia nanga katika moja ya bandari za Saudia.