Hatua isiyotosha ya Marekani ya kutia kasi mazungumzo ya Vienna
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i80046-hatua_isiyotosha_ya_marekani_ya_kutia_kasi_mazungumzo_ya_vienna
Baada ya serikali ya Marekani kutangaza kuondoa baadhi ya vikwazo ambavyo Washington ilikuwa imeiwekea Tehran, Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema kuwa, hatua hiyo haitoshi. Wizara ya Mambo ya nje ya Iran imesema, inachotakiwa kufanya Marekani ni kuondoa vikwazo vyake vyote vikiwemo vikwazo vya nyuklia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 06, 2022 05:58 UTC
  • Hatua isiyotosha ya Marekani ya kutia kasi mazungumzo ya Vienna

Baada ya serikali ya Marekani kutangaza kuondoa baadhi ya vikwazo ambavyo Washington ilikuwa imeiwekea Tehran, Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema kuwa, hatua hiyo haitoshi. Wizara ya Mambo ya nje ya Iran imesema, inachotakiwa kufanya Marekani ni kuondoa vikwazo vyake vyote vikiwemo vikwazo vya nyuklia.

Juzi Ijumaa tarehe 4 Februari, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitangaza kuondolewa baadhi ya vikwazo vya kiufundi vya nyuklia vinavyohusiana na vituo vya nyuklia vya Bushehr, Arak na kinu cha utafiti wa nyuklia cha Tehran.

Afisa mmoja wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba: Hatua hiyo ya Marekani imechukuliwa kwa lengo la kutia kasi mchakato wa mazungumzo ya kiufundi na si sahihi kuchukuliwa hatua hiyo kuwa ni ujumbe wa kuonesha kwamba Marekani imeamua kurejea kwenye mapatano ya nyuklia ya JCPOA.

Rais wa Marekani, Joe Biden

 

Ni jambo lililo wazi kwamba hatua hiyo ya Marekani haitokuwa na taathira yoyote katika vikwazo vya kiuchumi ambavyo ndivyo hasa Iran inavyotaka viondolewe. Kwani kwa mujibu wa uamuzi wa hivi sasa wa Marekani, vitisho vya kuziwekea vikwazo nchi na mashirikia ya kigeni yakiwemo ya Russia, China na nchi za Ulaya zinazoshirikiana kiufundi na Iran katika masuala ya nyuklia, vimeondolewa. Lakini serikali ya Washington imetangaza kuondolewa vikwazo katika zile sehemu tu ambazo zinaitia wasiwasi na kuishughulisha Marekani na upande wa Ulaya ulioko kwenye JCPOA na haudhamini matakwa yoyote ya asili ya Iran.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tangu mwanzoni kabisa mwa awamu mpya ya mazungumzo yake na kundi la 4+1 linaloundwa na nchi za Russia, China, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, ilitangaza kuwa imeingia kwenye awamu hiyo ya mazungumzo kwa lengo la kuhakikisha kuwa vikwazo vya kidhulma vya Marekani dhidi yake vinaondolewa. Sasa bila ya Iran kujiridhisha kuwa vikwazo hivyo vimeondolewa kweli, na maslahi ya taifa la Iran yamelindwa kikamilifu katika mapatano ya JCPOA, bila ya shaka yoyote Tehran haitokuwa tayari kutia saini makubaliano yoyote mapya.

Hossein Amir-Abdolahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, kinachopiganiwa na timu ya Iran katika mazungumzo ya Vienna ni kupatikana dhamana inayotakiwa katika pande zote za kisiasa, kisheria na kiuchumi; Marekani inapaswa kuonesha kivitendo nia yake njema.

Hossein Amir-Abdolahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

 

Hivi sasa timu zinazoshiriki mazungumzo ya nyuklia ya Vienna zimerejea katika nchi zao kwa ajili ya mashauriano. Inatarajiwa kuwa wiki hii timu hizo zitarejea tena Vienna kwa ajili ya mazungumzo, baada ya kupumzika kwa siku kadhaa. Suala la kutolewa dhamana za kweli za kuikinaisha Iran, lilikubaliwa rasmi na upande wa pili wa mazungumzo ya Vienna wiki kadhaa nyuma. Hata hivyo vipengee vya makubaliano hayo bado havijakamilika na timu za mazungumzo zitakaporejea Vienna wiki hii, zitajadiliana tena vipengee hivyo.

Kiujumla ni kwamba, kinachosubiriwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuiona Marekani inaheshimu na kutekeleza kivitendo ahadi zake za kuiondolea Iran vikwazo kwa mujibu wa mapatano ya JCPOA na inaamini kwamba kuondolewa vikwazo vya kidhulma vya kiuchumi vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Iran, kutatia kasi kufikiwa makubaliano mapya katika mazungumzo ya Vienna.

Saeed Khatibzadeh, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran naye amezungumzia jambo hilo na kusisitiza kuwa, hatua yoyote itakayochukuliwa katika njia ya kutekeleza mapatano ya nyuklia ya JCPOA itazingatiwa kwa kina na Tehran.