Iran: Uamuzi wa AU kuisimamishia Israel uanachama ni wa hekima, sahihi
Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepongeza uamuzi wa Umoja wa Afrika wa kusimamisha hadhi ya uanachama mtazamaji ya utawala wa Kizayuni Israel katika jumuiya hiyo ya kibara.
Saeed Khatibzadeh, Msemaji wa wizara hiyo amesema uamuzi huo wa Umoja wa Afrika wa kuusimamisha utawala wa Kizayuni kuwa mwanachama mwangalizi katika Umoja wa Afrika ni sahihi na wa hekima.
Khatibzadeh amesema kitendo hicho cha AU na nchi wanachama kimetangaza wazi msimamo wa umoja huo wa kutorodhishwa na mienendo ya utawala wa ubaguzi wa rangi wa Israel. Ameeleza bayana kuwa, kadhia ya Palestina ni yenye thamani kubwa na inayoungwa mkono na wapenda haki na uhuru katika pembe zote za dunia.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hatua hiyo ya AU imetuma ujumbe wa wazi kwa madola fulani ya Asia Magharibi, ambayo yamefanya mahesabu ghalati ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni.

Katika kikao chao cha juzi Jumapili huko Addis Ababa, Ethiopia, viongozi wa nchi za Afrika walisimamisha mjadala kuhusu kadhia ya uanachama mwangalizi wa Israel katika umoja huo, na kuunda kamati inayojumuisha wakuu wa nchi saba za Afrika, ikiwemo Algeria, kushughulikia suala hilo.
Aidha Syria, Harakati za mapambano ya ukombozi za Palestina za Hamas na Jihad Islami zimeushukuru Umoja wa Afrika kwa kuutimua utawala wa Kizayuni wa Israel kwenye umoja huo na kusema kuwa, hatua hiyo ni pigo kwa zile nchi zinazotangaza uhusiano wa kawaida na utawala huo katili.