Ebrahim Raisi: Iran bado imeshikamana na nara ya "Si Mashariki si Magharibi"
Rais Ebrahim Raisi amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran bado imeshikamana na nara yake ya "Si Mashariki, si Magharibi" ya tangu mwaka 1979.
Rais Raisi amesema hayo leo wakati akihutubia kilele cha maadhimisho ya Bahman 22, ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Mapinduzi ya Kiislamu yalifikia kwenye ushindi tarehe 11 Februari 1979 kwa uongozi wa mwanachuoni shujaa, Imam Khomeini MA.
Leo Ijumaa, wananchi wa Iran wameadhimisha mwaka wa 43 wa ushindi wa mapinduzi matukufu ya Kiislamu katika kona zote za nchi na wamejitokeza kwa wingi kwenye kilele cha maadhimisho hayo, ikiwa ni kuweka historia ya hamasa nyingine ya fakhari za Mapinduzi ya Kiislamu.
Mwaka huu maadhimisho hayo yamefanyika kwa kutumia pikipiki katika baadhi ya miji kama Tehran kutokana na wimbi la ugonjwa hatari wa kuambukiza wa UVIKO-19.
Mwishoni mwa maandamano ya leo, Rais Ebrahim Raisi ametoa hotuba kabla ya khutba za Sala ya Ijumaa hapa jijini Tehran na amesema kuwa, kinachopiganiwa muda wote wa Mapinduzi ya Kiislamu ni uhuru, maadili bora, busara, uadilifu, uhuru, heshima ya taifa, udugu na kutokubali kuwa chini ya dhulma na ubeberu.
Amesema, Mapinduzi ya Kiislamu yalitokea nchini Iran ili kuusambaratisha utawala muovu na kibaraka wa madola ya kibeberu na yalifanikiwa kutokana na uungaji mkono mkubwa sana wa wananchi.
Amesema, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yamejengeka juu ya msingi wa kupigania uadilifu na haiwezekani kabisa kuyavua mapinduzi hayo matukufu na sifa hiyo ya uadilifu kwani kupigania uadilifu na kusimama dhidi ya dhulma na ufisadi ni sifa zilizokita mizizi ndani ya Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran.