Mapinduzi ya Kiislamu na kusambaratika satwa ya madola ya kiistikbari duniani
Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran tarehe 11 Februari 1979 ulikuwa tukio muhimu na la kipekee katika historia ya maelfu ya miaka ya Iran. Haya ni mapinduzi ambayo yalipelekea kuibuka mabadiliko ya kimsingi katika jamii ya Iran katika nyanja za kisiasa, kijamii, kiuchumi na kiutamaduni.
Pamoja na hayo, moja kati ya matukio yaliyokuwa na taathira katika Mapinduzi ya Kiislamu ni kuibuka mwelekeo mpya katika sera za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hizo ni sera ambazo zimejengeka katika msingi wa kukabiliana na madola ya kiistikbari na kibeberu.
Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaeleza hayo katika ibara mbalimbali. Ibara ya 2 kipengee c, inapinga dhulma ya aina yoyote na ukandamizaji na ubeberu, na ibara 3 kipengee 5, kinapinga kabisa ukoloni na kupiga vita ushawishi wa kigeni.
Manouchehr Mohammadi, profesa wa sayansi ya kisiasa anasema: "Heshima, hekima na maslahi" zimekuwa kanuni tatu kuu na zisizobadilika ambazo msingi wake umeunda siasa za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi amezitaja kanuni hizo tatu kuwa ni pembetatu muhimu kwa mfumo wa mahusiano ya kimataifa na kueleza kuwa maingiliano ya Iran na walimwengu katika waraka wa dira ya miaka 20 ya nchi yatatekelezwa kwa kuzingatia misingi hiyo mitatu."
Kwa kuzingatia taathira za kieneo na za kimataifa za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, tangu mwanzoni kabisa mwa ushindi wake, madola ya kiistikbari duniani ambayo kinara wao ni Marekani na washirika wake wa kieneo, yalianza kuipinga Jamhuri changa ya Kiislamu na kujaribu kuiangusha.
Miongoni mwa vielelezo vya uadui huo ilikuwa ni kuhimizwa kwa utawala wa Baath nchini Iraq kuivamia Iran ya Kiislamu mnamo Septemba 1980, na kuanzishwa vita vya kulazimishwa vilivyoendelea kwa miaka minane. Wakati wa vita hivyo, madola makubwa ya kiistikbari na kibeberu ya Mashariki na Magharibi yalitoa aina mbalimbali za silaha, taarifa za kijasusi na misaada ya kisiasa kwa dikteta wa Iraq, Saddam Hussein. Hata hivyo, katika kivuli cha umoja wa kitaifa, imani na moyo wa kujitolea kufa shahidi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilisimama kidete kukabiliana na uvamizi huo na hatimaye kuibuka na ushindi.
Katika miongo mitatu iliyopita, kutokana na kuenea ujumbe wa Mapinduzi ya Kiislamu nje ya nchi na kustawi ushawishi wa kieneo wa Iran, Marekani ikiwa kinara wa kambi ya Magharibi, daima imekuwa ikifanya juhudi kubwa zaidi za kuzidisha uadui na Iran na kujaribu kuidhoofisha kwa kutumia mbinu laini na zisizo laini kama vile vita vya kisaikolojia na kipropaganda hasa katika vyombo vya habari, vikwazo vikubwa zaidi na visivyo na kifani dhidi ya Iran, na kitisho cha kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya Iran.
Licha ya juhudi na hatua hizo za kiuadui, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hivi sasa iko katika nafasi ya juu kabisa ya kieneo na ina nafasi nzuri sana na yenye taathira katika medani ya kieneo. Hili daima limekuwa ni moja ya matakwa makuu ya Washington kutoka kwa Iran, hususan katika muongo mmoja uliopita, la kutaka kubadilisha sera za kieneo za Iran.
Hili linaonyesha ni kwa kiasi gani sera na hatua za Tehran hususan uungaji mkono wake kwa harakati za kupinga uistikbari na Uzayuni kutoka Yemen hadi Lebanon, Palestina, Iraq na Syria zilivyotoa pigo kwa sera za kivita za Marekani na washirika wake wa kieneo.
Katika upande mwingine, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni miongoni mwa nchi zenye ufanisi katika kuchagiza mielekeo ya kimataifa kutokana na diplomasia yake mahiri na amilifu na uhusiano wake na nchi zinazopinga utawala wa Kizayuni kutoka Asia hadi Amerika ya Kusini.

Kwa kuzingatia mtazamo wa uhasama wa nchi za Magharibi dhidi ya Iran, ambao ulidhihirika katika hatua ya Marekani ya kujitoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA katika kipindi cha utawala wa Donald Trump na kutumia siasa za mashinikizo ya juu dhidi ya Iran, Tehran inataka kuleta mlingano katika sera za kigeni sambamba na kusambaratisha njama za madola ya Magharibi. Ni kwa msingio huo ndio Iran ikaamua kufuata sera za kuelekea upande wa mashariki na kupanua uhusiano wake na Uchina na Russia ambazo ni wapinzani na mahasimu wa Marekani duniani. Sera kama hii itafanikisha zaidi mchakato na azma ya Iran ya kusmabaratisha vikwazo vya Marekani dhidi yake. Aidha uhusiano wa kariibu wa Iran na madola yanayopinga ubbeberu dunani kama vile Venezuela na Cuba ni jambo ambalo litaibua fursa mpya za kiuchumi na kisaisa sambamba na kusambaratisha njama za Marekani za kuitenga Iran kimataifa
Hivi sasa, miaka 43 baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Jamhuri ya Kiislamu inatambuliwa na weledi wa mambo kuwa taifa muhimu la kieneo na mhusika mwenye ushawishi katika uga wa kimataifa.
Akizungumzia nafasi ya Iran katika eneo, Mohammad Odeh Al-Agha, mtaalamu wa masuala ya Asia Magharibi amesema: Iran kwa kuwa na nafasi yake ya kipekee ya kijiografia katika Ghuba ya Uajemi, imethibitisha mara kwa mara kuwa ni taifa lenye ushawishi mkubwa zaidi katika eneo hili."