Rais Ebrahim Raisi: Gesi asilia itaunda mustakbali wa nishati duniani
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika Mkutano wa Jumuiya ya Nchi Zinazouza Nje Gesi Asilia (GECF) kwamba gesi asilia inaunda mustakbali wa nishati ya dunia na ni chanzo muhimu cha nishati kwa ajili ya jamii.
Rais Ebrahim Raisi ameyasema hayo katika Mkutano wa Sita wa Jumuiya ya Nchi Zinazouza Nje Gesi Asilia (GECF) ulioanza rasmi asubuhi ya leo (Jumanne) ukihudhuriwa na wakuu na wawakilishi wa nchi wanachama ambao umefunguliwa kwa hotuba ya Amir wa Qatar kwa kaulimbiu ya "Usalama wa Nishati Duniani".
Mkutano huo unahudhuriwa na marais wa nchi, mawaziri wakuu na mawaziri wa nishati wa Iran, Algeria, Misri, Libya, Nigeria, Qatar, Russia, Venezuela, Trinidad na Tobago, na wajumbe waangalizi wakiwemo wa Azerbaijan, Iraq, Malaysia, Norway, Peru na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Sayyid Ebrahim Raisi amesema katika hotuba yake kwenye mkutano huo kwamba nchi zenye akiba kubwa na wauzaji nje wa gesi asilia zinatangaza waziwazi ujumbe wao kwa dunia kwamba lengo ya jumuiya hiyo ni kulinda haki ya mamlaka ya nchi wanachama na ushirikiano zaidi kwa ajili ya ugunduzi wa gesi asilia.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa: "Katika hali inayoikabili dunia kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa corona, nashauri gesi asilia ihudumie uchumi wa dunia katika kipindi cha ya baada ya corona."
Amesema “Kama nchi zenye hifadhi kubwa na wauzaji gesi nje ya nchi, ili kuboresha usalama wa mahitaji ya gesi asilia kwa kutekeleza malengo na dhamira ya GECF, tunaweza kutuma ujumbe wa wazi kwa dunia wa kuhakikisha upatikanaji wa nishati endelevu kwa kipindi kifupi na kirefu."
Rais wa Iran amesema: "Gesi asilia, ambayo ni nishati safi na salama itachangia sehemu kubwa ya matumizi ya nishati duniani kwa miongo kadhaa ijayo, na itaendelea kuwa na faida za kiuchumi, kiufundi na kimazingira kuliko nishati nyingine."
Sayyid Ebrahim Raisi amesema: "Mtazamo wetu kama wajumbe wa Jumuiya ya Nchi Zinazouza Nje Gesi, kwa ajili ya kusambaza gesi asilia zaidi kwenye soko la dunia, ni mtazamo unaotilia maanani masuala ya kibinadamu."
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliwasili jana huko Doha mji mkuu wa Qatar kwa mwaliko wa Amir wa nchi hiyo, kuhudhuria Mkutano wa Sita wa Jumuiya ya Nchi Zinazouza Nje Gesi Asilia (GECF) sambamba na kuimarisha uhusiano wa pande mbili.
Jumuiya ya nchi zinazozalisha na kuuza kwa wingi gesi duniani, iliasisiwa mwezi Mei mwaka 2001 mjini Tehran; na kwa sasa ina nchi 11 wanachama na nchi sita wanachama waangalizi.