Iran yapinga kutumiwa vibaya haki za binadamu kwa malengo ya kibeberu
(last modified Thu, 03 Mar 2022 12:52:48 GMT )
Mar 03, 2022 12:52 UTC
  • Iran yapinga kutumiwa vibaya haki za binadamu kwa malengo ya kibeberu

Naibu wa Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya kimataifa ambaye pia ni Katibu wa Kamati ya Haki za Binadamu ya Iran amesema kuwa, Tehran inapinga vikali kutumiwa vibaya suala la haki za binadamu.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran Press, Kazem Gharib Abadi amesema hayo pambizoni mwa kikao cha 49 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva Usiwisi wakati alipoonana na Waziri wa Sheria wa Namibia, Bi Yvonne Dausab.

Gharib Abadi amezungumzia maendeleo makubwa ya haki za binadamu nchini Iran na taathira mbaya za hatua za kihalifu za magenge ya kigaidi pamoja na jinsi madola ya kibeberu ya magharibi yanavyotumia vibaya suala la haki za binadamu kuzishinikiza nchi huru duniani na kuongeza kuwa, vikwazo vya upande mmoja vinavyowekwa na nchi fulani kwa utashi wake tu dhidi ya mataifa mengine, ni uvunjaji wa wazi zaidi wa haki za binadamu za watu wa mataifa hayo wakiwemo wa taifa la Iran.

Yvonne Dausab, Waziri wa Sheria wa Namibia

 

Kwa upande wake Waziri wa Sheria wa Namibia ameelezea msimamo mkuu wa nchi yake wa kupinga vikwazo na ubeberu wa nchi za Magharibi dhidi ya nchi zinazoendelea ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema kuwa, vitendo kama hivyo vya nchi za kibeberu za Magharibi ni uvunjaji wa haki za binadamu na vina taathira mbaya katika juhudi za kuhakikisha haki ya kila mtu inalindwa.

Vile vile ameyalaumu madola ya Magharibi kwa kutumia vibaya suala la haki za binadamu na kusema kuwa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa ni chombo cha kiutaalamu na hakipaswi kufanya kazi zake kisiasa kwa hali yoyote ile.