Mazungumzo ya Vienna na umuhimu wa safari ya Grossi mjini Tehran
Rafael Grossi Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ta Atomiki (IAEA) leo Jumamosi amewasili hapa Tehran na kulakiwa na Behrouz Kamalvandi Msemaji na Mkuu wa Masuala ya Kimataifa wa Shirika la Nishati ya Atomiki lal Iran. Ziara ya Grossi hapa Tehran inafanyika kwa lengo la kuzipatia ufumbuzi baadhi ya hitilafu za mitazamo kuhusu faili la nyuklia la Iran pamoja na masuala mengine kati ya Iran na wakala wa IAEA.
Vilevile suala la kuendelezwa ushirikiano wa kiufundi kati ya Iran na wakala wa IAEA limepangwa kujadiliwa katika safari hii ya Rafael Grossi hapa Tehran.
Hii ni safari ya tatu ya Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) mjini Tehran katika kipindi cha serikali ya sasa ya Iran. Ziara hii ya Mkurugenzi Mkuu wa IAEA imefanyika kufuatia mazungumzo ya kina ya wiki kadhaa za karibuni kati ya maafisa wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran na wa wakala wa IAEA pamoja na mapatano kadhaa yaliyofikiwa hadi sasa.
Ziara ya Grossi mjini Tehran ina umuhimu mkubwa kwa kuzingatia kuwa, imefanyika huku mazungumzo ya Vienna yakiendelea kwa ajili ya kuindolea Iran vikwazo vya kidhulma, na mjadala mkubwa ukiendelea kuhusu baadhi ya masuala ambayo bado hayajapatiwa ufumbuzi. Hasa ikitiliwa maani kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel ambao umefanya juu chini kuvuruga mchakato wa mazungumzo ya Vienna hata kwa kutuma ujumbe wake nchini Austria, sasa na baada ya kugonga mwamba katika hilo, unataka kutumia fursa ya mwisho iliyosalia ili kufanikisha malengo yake ya uharibifu.
Iran inataka kutatua hitilafu baina yake ya wakala wa IAEA na kuhitimisha masuala yote yenye utata. Licha ya kuwa mazungumzo kati ya Iran na IAEA katika siku kumi zilizopita yalikuwa magumu sana na yenye changamoto nyingi lakini kulindwa uhusiano wa kitaalamu na ushirikiano endelevu kati ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia na Tehran katika siku za karibuni pamoja na ubunifu mkubwa uliodhihirishwa na pande mbili vimesaidia pakubwa kuendelezwa majadiliano kati ya pande hizo mbili. Ni wazi kuwa, masuala ya usalama kati ya Iran na IAEA ni kati ya vizuizi vikuu vinavyopelekea kusuasua mchakato wa mazungumzo ya Vienna; na iwapo safari hii ya Grossi itapelekea kufikiwa ramani ya njia ya pamoja kwa ajili ya kutatua masuala hayo ya usalama kati ya Iran na IAEA, basi tunaweza kuwa na matarajio ya kuondolewa moja ya vizuizi vikuu vinavyokwamisha kufikiwa mapatano katika mazungumzo ya sasa ya kuondoa vikwazo huko Vienna.
Ali Bigdeli mchambuzi wa masuala ya kimataifa anaashiria ziara ya Rafael Grossis hapa Tehran na kusema: Kwa kuzingatia kuwa mazungumo ya Vienna yanakaribia kumalizika, ziara hii ina umuhimu mkubwa, kwa sababu mapatano hayawezi kusainiwa kama wakala wa IAEA hautawasilisha ripoti nzuri kuhusu miradi ya nyuklia ya Iran kwa Bodi ya Magavana na kwa nchi wanachama katika mapatano ya JCPOA ."
Iwapo ripoti ya IAEA kuhusu miradi ya nyuklia ya Iran na suala la kusimamiwa na kukaguliwa vituo vya nyuklia itakuwa nzuri, tunaweza kusema kuwa, faili la mazungumzo ya Vienna hatimaye litafungwa; na pande mbili zitafikia mapatano. Kwa sababu hiyo ziara ya sasa ya Mkurugenzi Mkuu wa IAEA mjini Tehran imetathminiwa kuwa na umuhimu mkubwa. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikitilia mkazo nia yake njema ya kushirikiana na kufanya mazungumzo na wakala wa IAEA sambamba na kutekeleza majukumu yake katika fremu ya kanuni na miongozo ya wakala huo.