Jahromi: Marekani inasalia kuwa adui wa kudumu wa taifa la Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i82066-jahromi_marekani_inasalia_kuwa_adui_wa_kudumu_wa_taifa_la_iran
Msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema vikwazo vipya vya Washington dhidi ya raia wa Iran vinaonyesha wazi kuwa, Marekani inasalia kuwa adui wa kudumu wa taifa hili.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 02, 2022 08:35 UTC
  • Jahromi: Marekani inasalia kuwa adui wa kudumu wa taifa la Iran

Msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema vikwazo vipya vya Washington dhidi ya raia wa Iran vinaonyesha wazi kuwa, Marekani inasalia kuwa adui wa kudumu wa taifa hili.

Shirika la Iran Press limemnukuu Ali Bahadori Jahromi akisema hayo leo Jumamosi kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kueleza kuwa, vikwazo vipya dhidi ya taifa hili, na hatua ya Washington kumzuia muimbaji wa Iran, Alireza Ghorbani kuingia katika ardhi ya Marekani ambako alikuwa anasubiriwa kutumbuiza katika hafla ya Nowruz ya kukaribisha mwaka mpya wa Kiirani, ni ishara tosha kuwa US ni adui wa kudumu wa Wairani.

Jahromi ameeleza kuwa: Serikali ya Marekani ina rekodi iliyo wazi ya kuvunja mikataba, kukanyaga sheria za kimataifa na kukiuka haki za binadamu, na kwa mara nyingine tena Wamarekani wamedhihirisha uadui walionao dhidi ya taifa la Iran.

Msemaji wa serikal ya Iran amebainisha kuwa, maafisa wa Idara ya Uraia na Uhamiaji ya Marekani siku ya Ijumaa kwa kutumia visingizio visivyo na maana, walimkamata na kumsaili kwa saa kadhaa muimbaji wa Iran, Alireza Ghorbani aliyekuwa akitokea Toronto, kabla ya kufuta viza yake na kutomtuhusu kuingia nchini humo.

Machi 30, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani iliwawekea vikwazo shakhsia na taasisi kadhaa za Iran ikiwa ni katika kuendeleza hatua za kiuhasama za Washington dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. 

Marekani imewawekea vikwazo vipya raia kadhaa wa Iran katika hali ambayo siku kadhaa zilizopita viongozi wa serikali ya Rais Joe Biden walitoa madai mbalimbali kuhusu kufikia mapatano na Iran katika mazungumzo ya Vienna ya kuindolea Tehran vikwazo.