Iran: Afrika ni bara lenye fursa nyingi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i82074-iran_afrika_ni_bara_lenye_fursa_nyingi
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu ina azma thabiti na imejitolea kwa dhati kuona bara la Afrika linafanikiwa na kustawi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 02, 2022 22:24 UTC
  • Iran: Afrika ni bara lenye fursa nyingi

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu ina azma thabiti na imejitolea kwa dhati kuona bara la Afrika linafanikiwa na kustawi.

Saeed Khatibzadeh alisema hayo jana Jumamosi katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter baada ya kumaliza safari ya kuzitembelea nchi za Afrika Magharibi za Ghana na Sierra Leone.

Khatibzadeh amebainisha kuwa, "Nimekamilisha ziara ya kufana na ya kutia moyo barani Afrika, kwa kuzitembelea Ghana na Sierra Leone. Afrika ni bara lenye fursa nyingi za aina yake."

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amesema anaona fakhari kubwa kutokana na kuwepo kwa miongo kadhaa sasa ofisi za Shirika la Hilali Nyekundu la Iran na miradi mbalimbali ya maendeleo katika nchi za Afrika.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Iran ameeleza katika ujumbe wake wa Twitter kuwa: Kujitolea kwetu kuliona bara la Afrika lenye ufanisi kunasalia imara.

Kabla ya kuzitembelea nchi mbili hizo, Khatibzadeh aliitembelea Senegal na kukutana na kufanya mazungumzo na maafisa wa serikali ya Dakar na viongozi wa jumuiya za kijamii za nchi hiyo. Akiwa Dakar, alisema bara la Afrika lina nafasi ya juu kabisa katika siasa za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.