Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran asisitiza kuimarishwa uhusiano na Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i83922-waziri_wa_mambo_ya_nje_wa_iran_asisitiza_kuimarishwa_uhusiano_na_afrika
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amekutana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini na kusema: "Iran haina vizingiti vyovyote katika kustawisha uhusiano na Afrika Kusini na hasa serikali mpya ina azma ya kuimarisha zaidi uhusiano na nchi za Afrika."
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 23, 2022 02:40 UTC
  • Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran asisitiza kuimarishwa uhusiano na Afrika

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amekutana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini na kusema: "Iran haina vizingiti vyovyote katika kustawisha uhusiano na Afrika Kusini na hasa serikali mpya ina azma ya kuimarisha zaidi uhusiano na nchi za Afrika."

Candith Mashego-Dlamini Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini ambaye anaongoza ujumbe wa ngazi za juu mjini Tehran kwa lengo la kushiriki katika Kikao cha 10 cha Kamati ya Pamoja ya Ushauriano wa Kisiasa wa Iran na Afrika Kusini jana alasiri alikutana na kufanya mazungumzo na Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran.

Katika mazungumzo hayo, Amir-Abdollahian alisisitiza kuwa Iran ina mtazamo maalumu kuhusu Afrika Kusini na kwamba nchi hizi mbili zina uwezo mzuri wa kuimarisha uhusiano. Amesema kufanyika Kikao cha 15 cha Tume ya Pamoja ya Iran na Afrika Kusini baadaye mwaka huu mjini Pretoria kutakuwa na umuhimu mkubwa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran akimpokea Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini

Aidha ameishukuru Afrika Kusini kutokana na sera zake  kuhusu eneo la Asia Magharibi hasa msimamo wake wa kuunga mkono mapambano ya watu wa Palestina.

Naye Candith Mashego-Dlamini Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini amebainisha matumaini yake kuwa, kikao cha kamati ya pamoja ya kisiasa kitakuwa na mazungumzo mazuri kuhusu maudhui mbali mbali na kuainisha ramani ya njia ya ushirikiao wa nchi mbili.