Raisi: Vikwazo vipya vinaonesha Iran ina haki ya kutoiamini Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i84850-raisi_vikwazo_vipya_vinaonesha_iran_ina_haki_ya_kutoiamini_marekani
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hatua ya Marekani kwa upande mmoja kudai kuwa ina nia ya kweli ya kufanya mazungumzo na Iran na wakati huohuo inatangaza vikwazo vipya dhidi ya taifa hili kwa upande mwingine, inaonesha wazi kuwa Tehran ina haki kutoiamini Washington.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 17, 2022 07:25 UTC
  • Raisi: Vikwazo vipya vinaonesha Iran ina haki ya kutoiamini Marekani

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hatua ya Marekani kwa upande mmoja kudai kuwa ina nia ya kweli ya kufanya mazungumzo na Iran na wakati huohuo inatangaza vikwazo vipya dhidi ya taifa hili kwa upande mwingine, inaonesha wazi kuwa Tehran ina haki kutoiamini Washington.

Rais Ebrahim Raisi wa Iran amesema hayo leo Ijumaa hapa Tehran akihutubia mkutano uliopewa anuani ya 'Ustawi na Jihadi' na kuongeza kuwa, Wamarekani wamekiri wenyewe kuwa sera yao ya mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya Iran imefeli, na hivi sasa wanajaribu kuibana Jamhuri ya Kiislamu kupitia vikwazo.

Sayyid Ebrahim Raisi ameeleza bayana kuwa, ni jambo la kushangaza namna Marekani kwa upande mmoja inaitisha mazungumzo, na kwa upande wa pili inaendelea kurefusha orodha yake ya vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Rais wa Iran amesisitiza kuwa: Hatuiamini Marekani, walivunja ahadi zao. Nguvu za Marekani zinafifia, hivi sasa wanajaribu kutuweka chini ya mashinikizo kupitia vikwazo; je vikwazo hivyo vitaweza kutubana?

Raisi amesema taifa la Iran limekuwa chini ya vikwazo kwa zaidi ya miongo minne sasa, lakini wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu wamevigeuza vikwazo hivyo kuwa fursa ya kuistawisha zaidi nchi yao.

Rais Raisi amesema dunia inapaswa kutambua haki ya Iran ya kutoiamini Marekani kwa kuwa dola hilo lina misimamo ya kukinzana na hulka ya kukiuka ahadi zake. Ameongeza kuwa, Iran ipo katika njia ya kustawi kutokana na kushindwa vibaya sera ya mashinikizo na vikwazo ya Marekani.

Jana Alkhamisi, Wizara ya Hazina ya Marekani ilitangaza vikwazo dhidi ya sekta ya petrokemikali ya Iran, na vilevile dhidi ya kampuni za China, Imarati na India zinazotuhumiwa kufanikisha kuuzwa mafuta ya Iran nje ya nchi.

Hata hivyo Mehdi Safari, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na Diplomasia ya Uchumi amesisitiza kuwa, vikwazo hivyo vipya vya Marekani havitaizuia Jamhuri ya Kiislamu kuendelea na shughuli zake za kila siku.