Iran: Tutaendelea na mazungumzo bila ya kufumbia macho haki zetu zilizo wazi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i84862-iran_tutaendelea_na_mazungumzo_bila_ya_kufumbia_macho_haki_zetu_zilizo_wazi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu itaendelea na mazungumzo, haitatoka kwenye mkondo wa kuyafikisha kwenye tija mazungumzo hayo na haitofumbia macho haki zake zilizo wazi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 17, 2022 20:52 UTC
  • Iran: Tutaendelea na mazungumzo bila ya kufumbia macho haki zetu zilizo wazi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu itaendelea na mazungumzo, haitatoka kwenye mkondo wa kuyafikisha kwenye tija mazungumzo hayo na haitofumbia macho haki zake zilizo wazi.

Hossein Amir-Abdolahian amesema hayo katika mtandao wa kijamii wa Twitter na kuongeza kuwa, Tehran itaendelea na mazungumzo hayo kwa kuheshimu sheria ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) ambayo inahimiza kulindwa kikamilifu haki za taifa la Iran katika mazungumzo hayo.

Ameongeza kuwa, tunaitaka Marekani iangalie mambo katika uhalisia wake, iachane na wendawazimu wake wa vikwazo kama ambavyo tunautaka pia Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) utekeleza majukumu yake kiufundi na usichukue maamuzi kwa misukumo ya kisiasa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran vile vile amesema, Jamhuri ya Kiislamu haitoi nafasi ya wasiwasi na shaka yoyote ya kutoweza kufelisha vikwazo vya aina yoyote ile dhidi yake.

Rais wa Marekani, Joe Biden anaendeleza uraibu wa vikwazo wa nchi yake

 

Katika upande mwingine Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, hatua ya Marekani ya kudai kuwa ina nia ya kweli ya kufanya mazungumzo na Iran lakini wakati huohuo inatangaza vikwazo vipya dhidi ya taifa hili inaonesha wazi kuwa Tehran ina haki kutoiamini Washington.

Sayyid Ebrahim Raisi ameeleza bayana kuwa, ni jambo la kushangaza kuona Marekani inaitisha mazungumzo lakini wakati huo huo inaendelea na uraibu wake wa kurefusha orodha ya vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Rais wa Iran amesisitiza kuwa: Hatuiamini Marekani, walivunja ahadi zao. Nguvu za Marekani zinafifia, hivi sasa wanajaribu kutuweka chini ya mashinikizo kupitia vikwazo; je, vikwazo hivyo vitaweza kutubana?