Iran iko tayari kuipa Mali uzoefu katika sayansi, teknolojia na utafiti
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema iko tayari kuipa Mali tajriba na uzoefu wake katika nyuga za sayansi, teknolojia na utafiti.
Hayo yamesemwa na Mohammad-Ali Zolfigol, Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Utafiti wa Iran katika mazungumzo yake hapa mjini Tehran na Amadou Keita, Waziri wa Elimu ya Juu na Utafiti wa Kisayansi wa Mali, ambaye anaongoza ujumbe wa ngazi ya juu wa nchi yake katika safari rasmi ya kikazi hapa nchini.
Zolfigol amesema Jamhuri ya Kiislamu ina azma ya kuimarisha ushirikiano wake na nchi rafiki ya Mali, na kulifanya taifa hilo la Afrika Magharibi litimize ndoto zake za kustawisha sekta yake ya sayansi.
Amebainisha kuwa: Iran inaunda asilimia moja tu ya jamii ya watu wote duniani, lakini inamiliki asilimia 2 ya uzalishaji katika uga wa sayansi duniani, na ni miongoni mwa mataifa yanayoongoza ulimwenguni katika nyuga nyingi za sayansi, kama teknolojia ya nyuklia, sekta ya ulinzi, nanoteknolojia, bayoteknolojia, kemia n.k.
Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Utafiti wa Iran ameongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ina Vyuo Vikuu 140 na makumi ya taasisi za sayansi na teknolojia, na kwamba Tehran ipo tayari kuipa Mali uzoefu wake katika uga huo ili sekta yake ya elimu istawi zaidi.
Kwa upande wake, Amadou Keita, Waziri wa Elimu ya Juu na Utafiti wa Kisayansi wa Mali, ameashiria kuwa Mali ina Vyuo Vikuu 5 tu na kusisitiza kuwa, nchi hiyo ina hamu ya kustafidi na uzoefu wa Iran kwa ajili ya ustawi wa sayansi na teknolojia wa nchi hiyo ya Kiafrika.