Spika Qalibaf: Marekani ni mtekelezaji wa sera za Wazayuni katika eneo
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, Marekani ni mtekelezaji wa siasa na sera za Wazayuni katika eneo.
Tarehe 13 Julai, rais wa Marekani Joe Biden ataanza ziara yake katika eneo la Asia Magharibi, ambapo siku ya Jumamosi ya tarehe 16 atahitimisha ziara yake hiyo kwa kuitembelea Saudi Arabia.
Mohammad Baqir Qalibaf, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ameeleza katika hotuba ya ufunguzi wa kikao cha leo cha bunge hilo la Iran kwamba, kugeuzwa mtekelezaji wa sera za Israel katika eneo litakuwa kosa la kistratejia kufanywa na rais Joe Biden wa Marekani, na litakuwa na madhara kwa yeye mwenyewe kwanza kabla ya mtu yeyote yule.
Kuhusiana na safari hiyo atakayofanya Biden katika eneo, Qalibaf ameongeza kuwa, safari ya Biden inaendana kikamilifu na matakwa ya Wazayuni; na rais wa Marekani ni mtekelezaji wa ratiba na mipango ambayo hata ufafanuzi wa vipengee vyake pia umeratibiwa na kuainishwa na utawala wa Kizayuni ambao ndiye adui mkuu wa mataifa ya eneo hili.
Spika wa Bunge la Iran amesema, Israel ni utawala haramu na mvuruga uthabiti, ambao hauna uwezo wa kuongoza na kudhibiti hata hali yake ya ndani ya kisiasa.
Halidhalika, Qalibaf ametanabahisha na kutoa indhari kwa kusema: nchi za eneo ambazo zina historia na mustakabali wa pamoja na Iran inapasa ziwe macho mno na kutathmini kwa makini na kwa usahihi matokeo hasi ya mpango wowote unaoratibiwa kwa pamoja na Marekani na Israel, ambao lengo lake si jengine isipokuwa kuvuruga uthabiti na nidhamu katika eneo hili.../