Jun 09, 2016 14:04 UTC
  • Iran kuishtaki Saudia katika mahakama ya kimataifa juu ya maafa ya Mina

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema itaushtaki utawala wa Saudi Arabia katika mahakama ya kimataifa kutokana na vifo vya mamia ya mahujaji wa Kiiarani wakati wa maafa ya Mina mwaka jana.

Mostafa Pourmohammadi, Waziri wa Sheria wa Iran amesema tayari wamenakili malalamishi kutoka kwa familia za wahanga wa tukio hilo na kwamba vyombo vya dola vinajiandaa kuishtaki serikali ya Riyadh katika mahakama ya kimataifa kutokana na maafa hayo ya kizembe. Amesema kuwa kesi hiyo inaihusu nchi nyingine na kwa msingi huo haiwezi kusikilizwa na mahakama za hapa nchini, kwa hivyo kesi hiyo itawasilishwa katika mahakama ya kimataifa.

Hata hivyo, Waziri wa Sheria wa Iran amekiri kuwa changamoto inayowakabili juu ya kesi hiyo, ni hulka ya utawala wa kifalme wa Saudia kutoheshimu sheria na vyombo vya kimataifa.

Ibada ya Hija ya mwaka jana iliambatana na matukio mengi machungu na mbali na maafa ya Mina, kuanguka winchi ndani ya Masjidul Haram huko Makkah pia kulisababisha vifo vya mahujaji zaidi ya 100. Mahujaji zaidi ya 460 wa Kiirani walipoteza maisha katika matukio hayo yaliyosababishwa na uzembe na usimamizi mbaya wa ibada tukufu ya Hijja.

Tags