Waziri wa Ulinzi wa Iran ametaka kupambana kwa dhati na ugaidi
Waziri wa Ulinzi wa Iran amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa ni mhimili wa utulivu na usalama katika eneo la Mashariki ya Kati inaamini kuwa mapambano ya dhati na ya pande zote dhidi ya makundi ya kigaidi kwa minajili ya kurejesha amani na utulivu katika eneo na duniani kwa ujumla ni jukumu la kibinadamu.
Brigedia Jenerali Hossein Dehqan aidha amesema mwanzoni mwa kikao cha pande tatu cha Mawaziri wa Ulinzi wa Iran, Russia na Syria kilichofanyika jana hapa Tehran kuwa hali mbaya ya mambo inayolikabili eneo hili imesababishwa na siasa za kupenda kujitanua na kichokozi za Marekani, Israel na baadhi ya pande nyingine zinazounga mkono ugaidi na kuongeza kuwa: Iran siku zote inaunga mkono juhudi za kupatiwa ufumbuzi mgogoro wa Syria kwa njia ya mazungumzo baina ya Wasyria wenyewe.
Brigedia Jenerali Dehqan amesema, Iran inaamini kuwa ugaidi na migogoro inayozikabili Syria, Iraq, Yemen na maeneo mengine ya dunia inaweza kukomeshwa na kupatiwa ufumbuzi iwapo kutakuwa na mapambano ya kweli dhidi ya magaidi na kukata kikamilifu njia za kuwasaidi kifedha na kisiasa magaidi hao.