Uingereza na kuendelea kuingilia masuala ya ndani ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i89190-uingereza_na_kuendelea_kuingilia_masuala_ya_ndani_ya_iran
Balozi wa Uingereza nchini Iran ameitwa kwa mara ya tatu kwenda kusailiwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu na hiyo ni katika kipindi cha wiki tatu tu zilizopita. Hii ni kutokana na Uingereza kujitia kwenye uraibu wa kuiwekea vikwazo vya kiholela Iran. Tehran inasema, ina haki ya kulipiza kisasi siasa hizo za kiibeberu za London.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 12, 2022 05:26 UTC
  • Uingereza na kuendelea kuingilia masuala ya ndani ya Iran

Balozi wa Uingereza nchini Iran ameitwa kwa mara ya tatu kwenda kusailiwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu na hiyo ni katika kipindi cha wiki tatu tu zilizopita. Hii ni kutokana na Uingereza kujitia kwenye uraibu wa kuiwekea vikwazo vya kiholela Iran. Tehran inasema, ina haki ya kulipiza kisasi siasa hizo za kiibeberu za London.

Siku ya Jumatatu, serikali ya Uingereza ilikiwekea vikwazo kikosi cha usalama wa kimaadili cha Jeshi la Polisi la Jamhuri ya Kiislamu pamoja na maafisa kadhaa wa ngazi za juu wa kiusalama na kisiasa wa Iran; ikiwa ni kutangaza waziwazi London uungaji mkono wake kwa machafuko na mashambulio ya kigaidi yaliyofanywa na maadui wa taifa la Iran hivi karibuni.  Baada ya hatua hiyo ya Uingereza, balozi wa nchi hiyo hapa Tehran, Simon Shercliff, ameitwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran kwa mara ya tatu katika kipindi cha wiki tatu ili kusailiwa na kulalamikiwa uingiliaji wa Uingereza katika masuala yasiyoihusu.

Kabla ya hapo Shercliff alikuwa ameshaitwa mara mbili Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, yaani tarehe 24 Septemba na tarehe 5 Oktoba kutokana na Uingereza kuruhusu vyombo vya habari vya lugha ya Kifarsi kutumia ardhi ya Uingereza kuchochea machafuko nchini Iran.

Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran mjini Tehran

 

Baada ya kutokea machafuko katika baadhi ya miji ya Iran ambayo kimsingi hasa yamechochewa na nchi za Magharibi na vibaraka wasaliti wa taifa lao wa ndani ya Iran, nchi za Magharibi ikiwemo Uingereza na Marekani kwa mara nyingine zimeshadidisha mashinikizo yao na kuingilia zaidi masuala ya ndani ya Iran. Lengo la madola hayo ya kibeberu liko wazi nalo ni kutumia fursa yoyote ile kuongeza mashinikizo ya kisiasa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa shabaha ya kufanikisha malengo yao ya kiistikbari.

Tab'an Uingereza ina historia ndefu ya kufanya njama dhidi ya taifa la Iran. Moja ya mifano ya wazi kabisa ni uchochezi wa London baada ya uchaguzi wa kipindi cha 10 cha Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uliofanyika mwaka 2009. Wakati huo Uingereza ilituma balozi wake mpya mjini Tehran aliyejulikana kwa jina la Simon Gass ili kuchochea machafuko humu nchini. Baada ya uchaguzi huo kulizuka fitna mpya humu nchini iliyochochewa na madola ya kibeberu. Timu iliyokuwa inachukua amri kutoka London ilihusika pakubwa katika fitna hiyo licha ya kwamba suala hilo lilikuwa ni la ndani ya Iran kikamilifu na halikuihusu kivyovyote vile Uingereza.  Wakati wa fitna hiyo, wafanyakazi kadhaa wa ubalozi wa Uingereza mjini Tehran walitiwa mbaroni wakiwa katikati ya wafanya ghasia; na wanadiplomasia wawili wa Uingereza walitimuliwa humu nchini.

Katika kipiindi cha wiki za hivi karibuni pia, serikali ya Uingereza imeendelea na siasa zake za kibeberu za kuingilia masuala ya ndani ya Iran na kuunga mkono waziwazi watu waliokuwa wanafanya ghasia. Sasa hivi pia London imeamua kuiwekea Iran vikwazo vipya baada ya kufeli njama zake na licha ya mabanda ya kipropaganda yanayoendesha kazi zao nchini Uingereza kufanya uchochezi mkubwa na waziwazi dhidi ya usalama wa wananchi wa Iran. Si hayo tu lakini pia London imeshindwa hata kutimiza wajibu wake wa kimataifa wa kuvidhamiinia usalama vituo vya kidiplomasia vya Iran nchini humo. Polisi wa serikali ya London wanadharau kutekeleza majukumu yao wakati maadui wa taifa hili la Kiislamu wanaposhambulia maeneo ya kidiplomasia ya Iran huko Uingereza.

Polisi wa Uingereza walivyoruhusu kushambuliwa kama hivi ubalozi wa Iran mjini London

 

David Miller, mtaalamu wa masuala ya kisiasa na kijamii wa nchini UIngereza anasema kuhusu misimamo ya hivi karibuni ya nchi za Magharibi dhidi ya Iran kwamba: Asili ya mambo yote hapa ni kwamba, nchi za Magharibi zilikuwa zimekusudia kuizidishia vikwazo Iran lakini zilikosa pa kuanzia ndio maana zimeamua kuanzisha machafuko nchini Iran. Wapinzani wa mapatano ya nyuklia ya JCPOA wanafanya njama za kila namna kuharibu mchakato wa mazungumzo hayo. Wapinzani hao wa JCPOA ndio waliofaidika na hali hiyo na hivi sasa wanaendeleza njama zao za kuifanya Iran itengwe.

Bila ya shaka ni kwa sababu hiyo pia ndio maana Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran akasisitiza kwa kusema: Tutasimama kidete na bila ya kutetereka mbele ya njama zozote za madola ya Magharibi na Marekani na vikwazo na mashinikizo yao mapya ambayo yanalenga kuilazimisha Iran ilegeze misimamo yake na kutoa upendeleo kwa madola hayo ya kibeberu