Oct 27, 2022 13:19 UTC
  • Ayatullah Ali Khamenei
    Ayatullah Ali Khamenei

Kufuatia tukio la kigaidi lililotokea katika Haram ya Hadhrat Ahmad bin Musa (Shah Cheragh) huko Shiraz, Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametuma salamu za rambirambi kwa familia zilizofiwa akisisitiza kuwa wahalifu waliohusika na jinai hiyo wataadhibiwa.

Katika ujumbe wake wa rambirambi, Ayatullah Khamenei amesema kuwa: Huzuni ya wafiwa wapendwa na kuvunjiwa heshima Haram ya Ahlul-Bait (as) havitafidiwa isipokuwa kwa kuchunguza chanzo cha maafa haya na kuchukua hatua madhubuti na ya busara ya kukabilia nacho.

Amsema: Jinai ya kutisha iliyofanyika katika Haram tukufu ya Hadhrat Ahmad bin Musa, amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake, ambayo imepelekea kuuawa shahidi na kujeruhiwa makumi ya wanaume, wanawake na watoto wasio na hatia, imezifanya nyoyo kuwa na huzuni.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: "Sisi sote tuna wajibu wa kumshughulika adui anayewasha moto wa vitina na vibaraka wake, wasaliti au wajinga na walioghafilika."

Amesema: Vyombo vya usalama, Mahakama hadi wanaharakati katika nyanja ya fikra na ulinganiaji na wananchi wote kwa ujumla, wanapaswa kuwa mkono mmoja dhidi ya mrengo unaoruhusu kupuuzwa na kudharauliwa maisha ya watu, usalama na matukufu yao.

Msikiti na Haram ya Ahmad bin Musa (as), Shiraz

Ayatullah Ali Khamenei ameashiria pia kwamba, taifa azizi la Iran na taasisi husika, bila shaka, zitashinda njama mbaya za maadui na kuongeza kuwa: "Natoa rambirambi zangu kwa familia zilizopatwa na msiba katika tukio hili, watu wa Shiraz na kwa taifa zima la Iran, na ninawaombea shifaa majeruhi kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu."

Itakumbukwa kuwa, watu wasiopungua 15 wakiwemo watoto wawili wameuawa huku 27 wakijeruhiwa katika shambulio la kigaidi la jana Jumatano mwendo wa saa 12 kasorobo jioni kwa saa za hapa nchini, katika Haram Tukufu ya Shah Cheragh mjini Shiraz, katika mkoa wa Fars kusini magharibi mwa nchi.

Hharam ya Ahmad bin Musa al Kadhim (as), Shiraz

Shah Cheragh, Ahmad bin Musa al Kadhim (as) ni miongoni mwa wajukuu wa Mtume wetu Muhammad (saw) ambaye aliuawa shahidi na watawala wa Bani Abbas na kuzikwa katika mji wa Shiraz. 

Tags