Jibu la Rais wa Iran kwa bwabwaja na njozi za Biden
Rais Sayyid Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika marasimu ya kukumbuka tarehe 13 Aban ambayo inaadhimishwa hapa nchini kama Siku ya Kitaifa ya Kupambana na Uistikbari Duniani kwamba: Marekani ina nafasi ya kwanza katika vita na umwagaji damu na inaangamiza na kuharibu maslahi ya mataifa mengine ili kujidhaminia maslahi yake. Rais wa Iran ameeleza hayo katika radiamali yake kwa matamshi ya Joe Biden ya kuuunga mkono ghasia na fujo nchini Iran.
Katika marasimu hayo, Rais Raisi alisema: "masaa machache yaliyopita nimefahamishwa kuwa Rais wa Marekani ametoa kauli yake hiyo labda kutokana na kuchanganyikiwa kwake."Rais wa Marekani amesema, wao wanapaswa kuikomboa Iran, lakini (mimi namwambia kwamba) Iran ilishakombolewa miaka 42 iliyopita, na wala haitakuwa chini ya ubeberu na udhibiti wenu. Sisi kamwe hatutakuwa gombe la kukamwa maziwa."
Rais wa Iran ametoa jibu hilo kali ikiwa ni radiamali yake kwa matamshi ya karibuni ya Rais Joe Biden wa Marekani. Biden akiwa katika kampeni kubwa ya uchaguzi ya kukusanya misaada ya kifedha kwa ajili ya mwakilishi wa chama cha Democrat katika jimbo la California, magharibi mwa Marekani mbele ya umati wa watu ambao walikuwa wamebeba mabango yaliyoandikwa maneno yanayowaunga mkono wafanyafujo hapa nchini amesema: "msiwe na wasiwasi, sisi tutaikomboa Iran. Waandamanaji hivi karibuni watafanikiwa kuwa huru".
Uropokaji huu mpya wa Biden ambao ni sawa na kuingilia wazi masuala ya ndani ya Iran na ni hatua iliyo kinyume na sheria za kimataifa imempelekea John Kirby Mratibu wa Mawasiliano ya Kistratejia wa Baraza la Usalama wa Taifa wa White House kujaribu kulainisha matamshi hayo ya Biden. Afisa huyo wa White House jana Ijumaa alisema mbele ya waandishi wa habari akijibu swali aliloulizwa na mwandishi mmoja wa habari kuhusu makusudio ya matamshi ya Biden kwamba: "Biden kwa mara nyingine tena amebainisha kuhusu mshikamano wake na wafanya maandamano nchini Iran; hatua zile zile ambazo zimechukuliwa tokea awali, yaani ni jukumu la wananchi wa Iran kujiletea mageuzi. Wananchi wa Iran wenyewe ndio wanaopasa kuamua kuhusu mustkabali wao."
Ni wazi kuwa, Marekani ambayo hadi sasa kwa mara kadhaa imezituhumu nchi hasimu na zile zinazopinga ubeberu wa Magharibi zikiwemo Russia na Iran kuwa zinaingilia masuala ya yake ya ndani ukiwemo uchaguzi wa nchi hiyo; mara hii Rais wa nchi hiyo anatamka na kuropoka waziwazi na bila ya kificho chochote akiingilia masuala ya ndani ya Iran kwa kutoa madai ya eti kuikomboa nchi hii. Jambo jingine linalojitokeza wazi katika uga huu ni kuwa je, Marekani iliyokuwa na ushawishi mkubwa nchini Iran kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu ilichukua hatua gani kwa ajili ya kuwakomboa wananchi wa Iran? Miongoni mwa hatua zilizotekelezwa na Washington ilikuwa ni kufanya mapinduzi tarehe 28 Mordad sawa na Agosti mwaka 1953 na kuandaa mazingira ya kudumisha utawala kibaraka wa Shah hadi mwaka 1979. Hasa ikizingatiwa kuwa, Marekani ndiyo iliyopelekea kuasisiwa Shirika la Ujasusi la Shah (SAVAK) ambalo lilikuwa na nafasi na mchango mkuu katika kuwatia nguvuni na kuwauwa wanamapambano waliokuwa wakipigana dhidi ya utawala wa Pahlavi hadi kupatikana ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Katika upande mwingine, makampuni ya mafuta ya Kimarekani pia yalihusika pakubwa katika kuiba mafuta ya Iran katika miaka kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu; na wakati huo huo Marekani kwa kuitumia serikali ya Shah kama wenzo ilijikabidhi mamlaka ya kusimamia kikosi cha usalama wa eneo la Ghuba ya Uajemi kwa gharama ya taifa la Iran.
Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu pia Marekani iliendeleza hatua zake za kiadui na kiuhasama dhidi ya mfumo wa Jamhuri ya Kislamu ya Iran katika kalibu ya siasa zake za kujitanua na kuiwekea Iran vikwazo katika miongo minne ya karibuni. Aidha hatua ya Marekani ya kuiwekea Iran vikwazo wakati wa utawala wa Rais wa zamani wa nchi hiyo Donald Trump baada ya nchi hiyo kujitoa kwa upande mmoja katika mapatano ya JCPOA na kuanzisha wenzo wa mashinikio ya kiwango cha juu zaidi dhidi ya nchi hii, ilichukua mwelekeo mpya ambao haujawahi kushuhudiwa.
Washington ililiwekea taifa la Iran vikwazo vikali zaidi kwa kutaraji kuwa Iran ingesalimu amri mkabala wa matakwa yasiyo ya kimantiki na haramu ya Marekani; vikwazo ambavyo kama ilivyokiri serikali ya Biden vimefeli na kugonga mwamba. Rais wa sasa wa Marekani Joe Biden pia ameshadidisha wenzo huo wa mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya Iran tangu aingie madarakani licha ya nara na shaari zake za huko nyuma; na mara kwa mara hutangaza vikwazo vipya dhidi ya Iran kwa visingizio mbalimbali. Marekani hivi sasa imejiweka kando na mazungumzo ya Vienna kwa kisingizio cha kuibuka ghasia na fujo nchini Iran huku ikitilia mkazo kuwa bega kwa bega na kuwaunga mkono waibua fujo. Viongozi wa nchi hiyo si tu wametoa matamshi ya uingiliaji tokea kuanza ghasia za karibuni hapa nchini bali wamewawekea vikwazo pia viongozi na taasisi kadhaa za Kiirani; na katika juhudi zao za karibuni kabisa dhidi ya Iran, Marekani na Albania zimeitisha kikao kisicho rasmi cha Baraza la Usalama dhidi ya Iran. Hata hivyo kikao hicho ambacho pamoja na kelele zote zilizopigwa kimegonga mwamba na hakijawa na matunda kwa waliokiitisha.