Iran: Rais wa Ukraine ajifunze kwa hatima ya viongozi walioitegemea US
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amepuuzilia mbali madai yasiyokuwa na msingi kwamba Tehran imeipa Moscow ndege zisizo na rubani kwa ajili ya kuzitumia katika vita dhidi ya Ukraine na kusisitiza kuwa, Rais wa Volodymyr Zelensky wa Ukraine anapaswa kupata somo kutokana na hatima iliyowafika viongozi mbalimbali waliotegemea misaada ya Marekani.
Nasser Kan’ani alisema hayo jana Alkhamisi hapa mjini Tehran na kueleza kuwa, taifa la Iran halijawahi na halitawahi kuupa silaha upande wowote katika mgogoro wa Ukraine.
Amesema, "Daima tunaheshimu mamlaka ya kujitawala nchi nyingine, ikiwemo Ukraine, lakini Bwana Zelensky anapaswa kufahamu kuwa, wakati utafika Iran ishindwe kuvumilia madai hayo yasiyo na msingi."
Kan'ani ameeleza bayana kuwa, "Zelensky anapaswa kujifunza kutokana na hatima iliyowafika viongozi mbalimbali waliotegemea misaada na uungaji mkono wa Marekani."
Juzi Jumatano, Zelensky alihutubia Kongresi ya Marekani na kukariri madai yasiyo na msingi kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran eti imeipa Russia ndege zisizo na rubani (droni) kwa ajili ya kuzitumia katika vita dhidi ya Ukraine.
Hivi karibuni, Brigedia Jenerali Muhammad Reza Ashtiani, Waziri wa Ulinzi wa Iran alisema kuwa, Kiev haijawasilisha ushahidi unaothibitisha madai kwamba Russia imetumia droni za Iran katika vita dhidi ya nchi hiyo.
Alisisitiza kuwa, ushirikiano wa kijeshi wa Jamhuri ya Kiislamu na Russia umekuwepo kwa miaka mingi lakini hadi sasa hakuna ushirikiano wa kutumiwa droni za Iran katika vita vya Ukraine.