Spika wa Bunge la Iran awatakia kheri Wakristo wanapoadhimisha Krismasi
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amewatumia ujumbe wa kheri Wakristo wa Iran na duniani kwa ujumla wakati huu wanapoadhimisha sherehe zao za Krismasi.
Mohammad Baqer Qalibaf amesema katika ujumbe alioutoa kabla ya kuanza kikao cha Bunge hii leo kwamba, anawatakia kheri Wakristo wa Iran na duniani kiujumla katika sherehe zao za kukumbuka kuzaliwa Nabii Isa mwana wa Maryam AS.
Spika wa Bunge la Iran amesema: Natoa mkono wa baraka kwa Wakristo na wapenda haki kote duniani na hasa raia wenzangu wa Iran wa dini ya Kikristo kwa mnasaba wa maadhimisho ya siku ya kuzaliwa Nabii Isa AS.
Kuna Wakristo zaidi ya 120,000 wanaoishi hapa nchini Iran. Akthari yao ni Waarmenia wanaofuata madhehebu ya Kikristo ya Othodoksi.
Wakristo kote duniani hii leo wanaadhimisha sikukuu yao ya Krisimasi wanayoinasibisha na siku ya kuzaliwa Nabii Isa Masih AS, sherehe ambazo hufanyika tarehe 25 Disemba kila mwaka.
Wakatoliki na Waprotestanti huadhimisha Krismasi Disemba 25, huku Waothodoksi wakiadhimisha kumbukumbu ya mazazi hayo ya Nabii wa Allah, Isa Masih (AS) Januari 7.
Isa Masih (AS) ni mmoja wa Mitume wakubwa wa Mwenyezi Mungu ambaye ametajwa kwa heshima na taadhima kubwa katika Qur'ani Tukufu, na inamtambulisha kama mmoja wa Manabii wakuu waliopewa Kitabu na sheria na Mwenyezi Mungu.