Abbas atahadharisha kuhusu uvamizi wa Wazayuni dhidi ya Wakristo wa Palestina
Mkuu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesisitiza kuwa kamwe hawatauruhusu utawala wa Kizayuni wa Israel kuwalenga Wakristo katika ardhi za Palestina.
Mahmoud Abbas amesema katika hotuba yake kwa mnasaba wa maadhimisho ya siku ya kuzaliwa Nabii Isa Masiih (as) kwa mujibu wa imani ya Wakristo kwamba: "Leo tunakabiliana na vitendo vya wavamizi katika ardhi ya Palestina kwa umoja, kushikamana na misingi ya kitaifa na ustahimilivu."
Akiashiria kwamba Wakristo ni sehemu ya taifa na ardhi ya Palestina, Abbas amesema: "Hatutakubali kamwe kuona wavamizi wakiendelea kuwalenga Wakristo katika ardhi yetu."
Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesisitiza udharura wa kukabiliana na vitendo vya kibaguzi vya utawala wa Kizayuni wa Israel vya kutaka kuharibu utambulisho wa kitaifa na kiutamaduni wa Kikristo na Kiislamu wa Palestina na ameitaka jamii ya kimataifa ikomeshe kimya chake na kukabiliana na jinai za utawala huo ghasibu.
Mahmoud Abbas ameashiria pia ukandamizaji unaofanywa na Israel dhidi ya raia wa Palestina, kuendelezwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni, kuwatimua Wapalestina katika nyumba na ardhi zao, na kuuawa shahidi mamia ya Wapalestina katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita na kusema: "Hatutasahau maumivu na mateso tunayohisi mioyoni mwetu kutokana na ukandamizaji huo.”