Kamanda wa Iran: Jibu kali linawasubiri wavamizi wa taifa hili
Naibu Mratibu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameonya kuwa, chockochoko zozote za maadui zinazolenga kuhujumu uhuru na mamlaka ya kujitawala nchi hii zitakabiliwa kwa jibu kali la kijeshi.
Admeli Habibollah Sayyari amesema hayo pambizoni mwa mazoezi makubwa ya kijeshi ya Iran yanayofanyika katika eneo pana la kistratejia linaloanzia mashariki mwa Lango Bahari la Hormuz hadi katika ncha ya kaskazini mwa Bahari Hindi.
Kamanda huyo wa ngazi ya juu wa Jeshi la Iran amesisitiza kuwa, kufanyika kwa mafanikio luteka hiyo ni tanbihi na onyo kwa maadui, kwamba yeyote atakayethubutu kuchukua hatua ghalati dhidi ya mamlaka ya Iran atakabiliwa kwa jibu kali litakalomfanya ajute.
Luteka hiyo inayovishirikisha vikosi mbalimbali vya anga, nchi kavu na majini vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliyopewa jina la 'Dhulfiqar 1401' ilianza usiku wa kuamkia Ijumaa iliyopita, chini ya kaulimbiu isemayo "Kujiamini, izza na usalama endelevu" kwa ajili ya kuupiga jeki uwezo wa kujihami wa vikosi vya Iran.
Naibu Mratibu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, kufanyika luteka hiyo kubwa ya jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kunadhihirisha uwezo mkubwa wa kijeshi wa taifa hili katika kubaliana na vitisho vya maadui.
Wakati huohuo, ndege zisizo na rubani (droni) za kivita za Jeshi la Majini la Iran zimesambaratisha maeneo ya "adui dhahania" kwa kupiga kwa ustadi mkubwa shabaha zilizokusudiwa.
Droni hizo zilizotumika kwenye maneva hayo ya Dhulfiqar 1401 za Arash, Bavar, na Ababil 5 zimetokea kwenye manowari ya kijeshi ya Sahand, kupiga kwa usahihi mkubwa shabaha zilizokusudiwa.