Jan 09, 2023 04:10 UTC
  • Jenerali Salami: Hakuna shaka tutalipiza kisasi cha mauaji ya Shahidi Soleimani

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) amesema Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu alivunja na kusambaratisha njama za maadui wa taifa hili, na kwamba wahusika wa mauaji yake wanapaswa kufahamu kuwa lazima Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itachukua hatua kujibu kitendo cha kigaidi cha kumuua shahidi kamanda huyo.

Meja Jenerali Hossein Salami, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema hayo jana Jumapili huko Kerman, kusini mashariki mwa Iran, mji alikokulia Shahidi Soleimani na kueleza kuwa, "Adui anatumia nguvu zote ili kuuteka ulimwengu wa Kiislamu, kuyadhoofisha Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran pamoja na uhuru na hadhi ya taifa hili."

Jenerali Salami ameongeza kuwa, maadui wanafanya juu chini ili kuyateka na kuyakalia kwa mabavu maeneo ya Waislamu, kuanzia mashariki mwa Mediterrania hadi mashariki mwa Afghanistan, lakini njama hizo zitafeli.  

Kamanda Salami ameongeza kuwa, mauaji ya kigaidi na hatua zingine ghalati zinazochukuliwa na maadui hazitakuwa na matunda mengine kwao isipokuwa kuyafanya Mapinduzi ya Kiislamu yasonge mbele kwa kasi zaidi.

Luteni Jenerali Soleimani, ambaye alikuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la SEPAH, Naibu Kamanda Jeshi la Kujitolea la Wananchi wa Iraq, Abu Mahdi al-Muhandis, na wanamapambano wenzao waliuawa shahidi katika shambulio la ndege zisizo na rubani za Marekani karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad mapema  Januari 3, 2020. Shahidi Soleimani alikuwa ameelekea Iraq kwa mwaliko rasmi wa serikali ya nchi hiyo.

Ikulu ya White House na Pentagon ilitangaza kuwa ilihusika na mauaji hayo ya kigaidi  na kuthibitisha kuwa shambulio hilo lilitekelezwa kwa maelekezo ya Rais wa Marekani wa wakati huo Donald Trump.

Meja Jenerali Hossein Salami, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, "Kosa la maadui la kumuua kigaidi Soleimani haliwezi kusameheka, tunalipiza kisasi kila siku, na hakuna shaka tutalipiza kisasi zaidi kwa waliotekeleza mauaji hayo karibuni."

Tags