Feb 02, 2023 02:12 UTC
  • Majibu makali ya Tehran kuhusu msimamo ulio dhidi ya Tehran wa Blinken

Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, siku ya Jumatatu alijibu upayukaji mpya wa baadhi ya viongozi wa Marekani na kusema kuwa, serikali ya Washington inaelewa vilvyo kwamba Iran haiwezi kufumbia macho uchokozi wa aina yoyote ile wa ardhi yake na lazima itatoa majibu makali kwa yeyote anayelichokoza taifa hili la Kiislamu.

Alisema, serikli ya Marekani inapaswa izingatie masuala ya sheria za kimataifa kabla ya kutoa vitisho vyake dhidi ya Jamhuri ya Kisialmu ya Iran na itilie maanani pia madhara ya kisiasa yanayoweza kusababishwa na upayukaji wa viongozi wa nchi hiyo. 

Jumapili wiki hii, Antony Blinken, Waziri wa Mambo ya Jje wa Marekani alidai kuwa, Joe Biden, rais wa nchi hiyo ameshikilia vilivyo msimamo wake wa kuizuia Iran kumiliki kile alichokitaja ni silaha za nyuklia na kuongeza kuwa, machaguo yote yako mezani kwa ajili ya kuizuia Iran isimiliki silaha hizo. Blinken pia alisema, mazoezi ya kijeshi na utawala wa Kizayuni wa Israel yanawaruhusu Wamarekani kujilinda na kwamba ujumbe wa luteka hizo ni kwamba Washington iko tayari kujibu uvamizi wowote ule.

Antony Blinken, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani 

Kwa miaka mingi Marekani imekuwa ikikariri na kurudiarudia madai yake ya kwamba Iran inafanya mpango wa kumiliki silaha za nyuklia bila ya kutoa ushahidi wowote ule. Hata mwezi Agosti mwaka jana pia, viongozi hao wa Marekani walirudia madai hayo hayo kuwa eti Joe Biden anafanya kila analoweza kuizuia Iran kumiliki silaha za nyuklia. Kabla ya hapo pia, Robert Malley, mjumbe maalumu wa Marekani katika masuala ya Iran alisisitiza kuwa Joe Biden yuko tayari kutumia chaguo la kijeshi kuizuia Iran kumiliki silaha za nyuklia.

Madai hayo yasiyo na mashiko yanatolewa mara kwa mara na viongozi wa Marekani katika hali ambayo mara chungu nzima Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikisisitiza kuwa, haina mpango wowote wa kumiliki silaha za nyuklia. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Iran amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu mara chungu nzima imethibitisha kuwa mradi wake wanyuklia na wa amani na ni wa kiraia kikamilifu na hata Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA umethibitisha mara chungu nzima kuwa Tehran haina mpango kabisa wa kumiliki silaha za atomiki. Mara kwa mara viongozi wa Iran wanasisitiza kwamba silaha zote za maangamizi ya umati zikiwemo za nyuklia, hazimo kabisa katika ratiba zao za kiulinzi kwani zinapingana na mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu. Hii ni katika hali ambayo katikati ya mwezi Novemba 2022, Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa ya Nishati ya Atomiki alijibu swali kuhusu uwezekano wa Iran kumiliki bomu la nyuklia akisisitza kuwa, IAEA haina ushahidi wowote wa kuthibitisha kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina lengo na shabaha ya kumiliki silaha hizo. Hata Mkurugenzi wa Shirika la Usalama wa Taifa la Marekani, Avril Haines, amesema wazi kuwa Washington haina ushahidi wowote wa kuthibitisha kuwa viongozi wa Iran wameamua kumiliki silaha za nyuklia.

Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa IAEA 

Amma suala ambalo daima Marekani na nchi za Ulaya pamoja na utawala wa Kizayuni linawatia wasiwasi ni kuzidi nguvu za nyuklia za Iran katika matumizi ya amani na ya kiraia. Ijapokuwa Wakala wa Kiamtaifa wa Nishati ya Atomiki umethibitisha kimaandishi na mara chungu nzima kuhusu usalama wa mradi ya nyukia wa Iran, lakini pamoja na hayo madola hayo ya kibeberu yanaendelea kupiga ngoma ya vita na kurudia madai yao hayo hayo yasiyo na ushahidi wowote ili kupotosha fikra za walio wengi duniani. Tab'ani viongozi wa ngazi za juu wa kisiasa na kijeshi wa Iran wamekuwa wakisisitiza mara kwa mara pia kwamba uchokozi wa aina yoyote ile dhidi ya Tehran utapata majibu makali na kumfanya mchokozi ajutie uchokozi wake.

Tags