Raisi: Uhusiano wa Iran na Zimbabwe ni wa kirafiki
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu, amesema uhusiano wa Iran na Zimbabwe baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu daima umekuwa wa kirafiki na unaendelea kuimarika.
Rais Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo leo mjini Tehran wakati alipopokea vitambulisho vya Bright Kupemba balozi mpya wa Zimbabwe nchini Iran na kuongeza kuwa, uhusiano wa nchi hizi mbili baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu umekuwa wa kirafiki na unazidi kuboreka. Aidha amesema Iran na Zimbabwe zina uwezo mkubwa ambao unaweza kutumika kuimarisha uhusiano wa pande mbili.
Raisi aidha ameashiria mabadilishano ya jumbe za kidiplomasia baina ya Iran na Zimbabwe na kutiwa siani nyaraka mbali mbali za uhusiano wa kibiashara na kiuchumi na kuongeza kuwa, utekelezwaji wa nyaraka hizi unaweza kuwa kipaumbele cha balozi.
Kwa upande wake Bright Kupemba balozi mpya wa Zimbabwe nchini Iran amesema ni jambo la kupigiwa mfano kuona namna Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilivyoweza kustawi pamoja na kuwa imewekewa vikwazo vingi.
Aidha amesema katika kipindi chake cha kuhudumu Tehran atajitahidi kutumia uwezo na fursa zilizopo na kuibua nyuga mpya za ushirikiano wa Iran na Zimbabwe.
Inafaa kuashiria hapa kuwa kikao cha tano cha kamisheni ya pamoja ya kiuchumi ya Iran na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilifanyika kwa muda wa siku tano kuanzia Februari Mosi mjini Tehran na kukamilika kwa kutiwa saini mapatano ya ushirikiano baina ya pande mbili.