Kufukuzwa wanadiplomasia wa Ujerumani: Hatua mkabala ya Tehran kukabiliana na Berlin
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetoa amri ya kufukuzwa wanadiplomasia wawili wa Ujerumani kutokana na kuingilia kwao masuala ya ndani ya nchi.
Hatua hiyo imekuja baada ya Ujerumani kukosoa uamuzi wa Jamhuri ya Kiislamu wa kutoa hukumu ya kifo kwa kiongozi wa kundi la kigaidi lenye makao yake makuu nchini Marekani, ambalo limetekeleza mashambulizi kadhaa ya kigaidi nchini.
Nasser Kana'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, alitangaza Jumatano kwamba wanadiplomasia hao wawili wa Ujerumani wametangazwa kuwa "watu wasiotakikana" na kuamriwa kuondoka nchini mara moja kutokana na hatua za kutowajibika na uingiliaji wa serikali ya Berlin katika masuala ya ndani ya nchi ikiwa ni pamoja na kuingilia masuala ya mahakama ya Iran.
Kanani amesema kwamba kipaumbele cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima ni kudumisha maingiliano katika mazingira ya heshima, lakini ikiwa baadhi ya pande zinataka kupuuza kanuni na mamlaka ya kitaifa ya Iran, baasi kuchukuliwa hatua kama hiyo ni jambo lisiloepukika.
Kana'ani amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itachukua hatua madhubuti dhidi ya wanaoingilia masuala ya ndani ya nchi huku akiashiria kuitwa kwa balozi wa Ujerumani mjini Tehran katika Wizara ya Mambo ya Nje ili kujulishwa uamuzi huo.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani ilitangaza katika taarifa siku chache zilizopita kwamba wafanyakazi wawili wa Ubalozi wa Iran huko Berlin wamefukuzwa nchini humo.
Uamuzi huo ulichukuliwa baada ya Mahakama ya Iran kumhukumu kifo raia wa Iran Jamshid Sharmahd ambaye pia ana uraia wa Ujerumani kwa kosa la kueneza ufisadi katika ardhi kwa kupanga na kuratibu vitendo vya kigaidi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock alitoa kauli isiyofaa baada ya kutolewa hukumu hiyo huku akiishutumu Jamhuri ya Kiislamu kwa kile alichodai ni "ukiukaji mkubwa wa haki za raia wa Ujerumani."
Sharmahd, ambaye pia ni mkazi wa Marekani, alikuwa kinara wa kundi la kigaidi la Tondar. Alishtakiwa kwa kupanga mfululizo wa mashambulizi, ikiwa ni pamoja na shambulio la mwaka 2008 dhidi ya kituo cha kidini katika mji wa Shiraz kusini mwa Iran, Mkoa wa Fars, ambalo liliua watu 14 na kujeruhi wengine zaidi ya 300.
Katika miongo miwili iliyopita, Sharmahd alianzisha shughuli zake kwa jina la 'Jumuiya ya Ufalme wa Iran' kwa kuzingatia maslahi ya utawala wa kifalme wa Pahlavi ulioangushwa Iran na kufanya jinai dhidi ya watu wa Iran kwa njia ya kuyavunjia heshima maeneo matakatifu na kufanya mashambulio ya kigaidi ikiwa ni pamoja na shambulio lililofanywa katika ukumbi wa kidini au Husseiniya ya Seyed al-Shohadah huko Shiraz.
Katika miaka ya hivi karibuni kundi hilo limekuwa likipanga na kutekeleza operesheni za kigaidi nchini Iran lakini mashirika ya usalama yamefanikiwa kugundua nyingi ya njama hizo kabla ya kutekelezwa.
Moja ya njama zilizokuwa zimepangwa na kundi hilo ni kushambulia maonyesho ya kimataifa ya vitabu ya Tehran ambayo huwa na msongamano mkubwa wa watu. Aidha inadokezwa kuwa kundi hilo la kigaidi la Tondar lilihusika katika mauaji ya shahidi "Masoud Alimohammadi", mmoja wa wanasayansi bingwa wa taaluma ya nyuklia nchini Iran.
Suala jingine muhimu ambalo linapaswa kutajwa kuhusu uadui wa Ujerumani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na watu wa Iran ni msaada mkubwa wa Berlin kwa utawala wa Baath wa Iraq katika miaka ya vita vya kulazimishwa dhidi ya Iran baina ya 1980-1988. Katika kipindi hicho Ujerumani iliupa utawala wa Bath wa Iraq msaada mkubwa wa silaha za kemikali au za sumu zilizotumika vitani. Makampuni 85 ya Ujerumani yalikuwa na nafasi muhimu sana katika kusambaza silaha za kemikali kwa utawala wa Baath wa Iraq ambazo zilitumika dhidi ya raia wa kawaida. Uungaji mkono huo wa Ujerumani ni moja ya sababu za kimya cha makusudi cha nchi za Magharibi kuhusu jinai hiyo. Ujerumani ilupatia utawala wa Saddam silaha za kemkiali katika hali ambayo ndiyo nchi pekee ambayo imetia saini Mkataba wa Geneva juu ya Marufuku ya Silaha za Kemikali na pia mkataba wa Umoja wa Ulaya wa kuzuia utengenezaji wa silaha za kemikali. Hivyo hatua hiyo ya Ujerumani ya kuupa utawala wa Saddam silaha za kemikali ni mfano wa wazi wa undumakuwili.
Mmoja wa wauzaji wakubwa wa mada za mabomu ya kemikali kwa utawala ulioangushwa wa Saddam nchini Iraq ni kampuni ya Ujerumani ya "Imhausen Chemical" na vyombo vya habari vya Ulaya, hasa vya Ujerumani, vimechapisha nyaraka nyingi kuhusu kadhia hiyo.
Ismail Baqaei Hamaneh, balozi wa zamani na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika mashirika ya kimataifa yenye makao yao makuu mjini Geneva, akikumbushia historia ya Ujerumani katika kuupa utawala wa Saddam silaha za kemikali za sumu na wajibu wa serikali ya Ujerumani katika suala hilo anasema: Watu wote waliohusika katika mradi wa kumpa silaha za sumu dikteta wa zamani wa Iraq, ni washirika katika kutenda uhalifu wa kivita wa Saddam.