Kan'ani: Ujerumani iombe radhi kwa jinai zake dhidi ya Iraq, Iran
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani matamshi yaliyotolewa na Annalena Baerbock, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu katika safari yake ya hivi karibuni nchini Iraq.
Katika taarifa, Nasser Kana'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema badala ya kubwabwaja, Ujerumani inapasa kuomba radhi kwa jinai zake za huko nyuma dhidi ya mataifa ya Iraq na Iran.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock alitoa kauli isiyofaa baada ya Iran kumhukumu kifo raia wa Iran Jamshid Sharmahd ambaye pia ana uraia wa Ujerumani, kwa kosa la kueneza ufisadi katika ardhi kwa kupanga na kuratibu vitendo vya kigaidi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu. Baerbock aliishutumu Jamhuri ya Kiislamu kwa kile alichodai ni "ukiukaji mkubwa wa haki za raia wa Ujerumani."
Kana'ani amesema matamshi ya Baerbock yanaonesha wazi kuwa Berlin inaunga mkono ugaidi na magenge ya watu wanaotaka kujitenga na Iran, na pia yanakusudia kuvuruga uhusiano wa Iran na Iraq.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema matamshi ya uropokaji yaliyotolewa na Baerbock akiwa Baghdad yalikusudia kuficha uungaji mkono wa Berlin kwa dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein katika vita vyake dhidi ya Iran mwaka 1980. Kana'ani amefafanua zaidi kwa kusema, Berlin iliipa serikali ya Baath silaha za kemikali ili izitumie dhidi ya wananchi ambao hawakuwa na ulinzi wa Iran.
Ameongeza kuwa, "Hivi sasa, idadi kubwa ya magaidi na makundi ya wanamgambo wanaotaka kujitenga na ambao mikono yao imejaa damu za Wairani na Wairaqi wampewa hifadhi nchini Ujerumani."
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema serikali na mataifa ya eneo la Asia Magharibi kamwe hayatasahau jinai za nchi za Magharibi ikiwemo Ujerumani za kuchochea vita na kuwaunga mkono madikteta katika eneo.