Kumalizika mkwamo wa miaka saba katika uhusiano wa Iran na Saudi Arabia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i94988-kumalizika_mkwamo_wa_miaka_saba_katika_uhusiano_wa_iran_na_saudi_arabia
Iran na Saudi Arabia zimekubaliana kuanzisha tena uhusiano kati ya pande mbili kwa upatanishi wa China baada ya mkwamo wa miaka saba.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 11, 2023 23:08 UTC
  • Kumalizika mkwamo wa miaka saba katika uhusiano wa Iran na Saudi Arabia

Iran na Saudi Arabia zimekubaliana kuanzisha tena uhusiano kati ya pande mbili kwa upatanishi wa China baada ya mkwamo wa miaka saba.

Wawakilishi wa Iran na Saudi Arabia wamesaini taarifa huko China kuhusu kuanza tena uhusiano wa pande mbili za Tehran na Riyadh katika kikao kilichohudhuriwa na Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, na Musaid bin Mohammed al Aiban mwenzake wa Saudia. Pande mbili zimekubaliana baada ya miezi miwili kuandaa mazingira ya kubadilishana mabalozi na kufungua tena balozi pamoja na mahitaji mengine kwa ajili ya kuhuisha uhusiano kati ya nchi mbili.  

Ali Shamkhani Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran na Musaid bin Mohammed al Aiban huko Beijing, China 

Riyadh ilikata uhusiano wake na Iran tokea mwaka 2016. Riyadh iliamua kukata uhusiano na Tehran kwa kisingizio cha kushambuliwa ubalozi na ubalozi wake mdogo mjini Tehran na katika mji wa Mash'had; kitendo ambacho kililaaniwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Sababu kuu iliyoipelekea Saudia kuchukua hatua hiyo ni sera za nje za Riyadh wakati huo dhidi ya Iran. Sera za kigeni za Saudia tangu 2015 hadi 2021 zilikuwa na sura ya kuhujumu dhidi ya nchi nyingine. Msimamo huo umetekelezwa makhsusi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na washirika wake katika miaka ya karibuni na hata Saudia ilikuwa sehemu muhimu ya siasa za Marekani za mashinikizo ya kiwango cha juu dhidi ya Iran.  

Kuanzia mwaka 2021 zimechukuliwa hatua mbalimbali kwa minajili ya kufufua uhusiano kati ya Riyadh na Tehran; na serikali ya zamani ya Iraq ilifanya jitihada za kupatanisha nchi mbili hizi. Hadi sasa tayari kumefanyika duru tano za mazungumzo kati ya wawakilishi wa Iran na Saudi Arabia huko Baghdad; ambapo viongozi wa Iran na Saudia wamesisitiza wazi ulazima wa kuhuisha uhusiano wao na hatimaye pande hizo zimesaini hati ya mapatano huko Beijing kwa upatanishi wa China.   

Kuhuishwa uhusiano wa Riyadh na Tehran ni kushindwa kwa Marekani na Israel. Kwa upande mmoja, suala hili muhimu limefikiwa huko Beijing tena kwa upatanishi wa China, nchi hasimu mkuu wa sasa wa Marekani duniani. Katika upande wa pili pia, mapatano hayo ni sawa na kufeli juhudi za Washington na Tel Aviv za kuibua hitilafu na mgawanyiko kati ya Saudia na Iran. Wakati huo huo, mapatano hayo ni pigo kwa staretejia ya Marekani na Israel ya kuidhihirisha Iran kama tishio hususan katika eneo la Magharibi mwa Asia.  

Suala jingine muhimu ni kwamba, mapatano yaliyofikiwa baina ya na Riyadh na Tehran kwa ajili ya kuhuisha uhusiano yatakuwa na athari muhimu pia kwa eneo zima la Magharibi mwa Asia. Kwa msingi huo, kutangazwa mapatano hayo ya Tehran na Riyadh kumeakisiwa pakubwa katika pembe mbalimbali duniani na kukaribishwa na nchi mbalimbali za kikanda. Hussein Amir- Abdollahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba: Kurejeshwa uhusiano wa kawaida kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Saudi Arabia kunazipa uwezo kubwa nchi mbili, kanda wa Asia Magharibi na Ulimwengu wa Kiislamu kwa ujumla. 

Hussein Amir- Abdullahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran 

Nukta nyingine muhimu hapa ni kuwa, kuhuishwa uhusiano kati ya Iran na Saudi Arabia kunadhihirisha sera za ujirani mwema za serikali ya awamu ya 13 ya Iran. Serikali ya awamu ya 13 inahimiza suala la kustawisha uhusiano na nchi za jirani na kanda ya Asia Magharibi katika fremu ya siasa za ujirani mwema. Hussein Amir- Abdollahian ameandika kuhusu suala hilo kwamba: Sera ya ujirani mwema, kama mhimili mkuu wa sera ya mambo ya nje ya serikali ya awamu ya kumi na tatu, inasonga mbele kwa nguvu katika mwelekeo sahihi.