Ushirikiano wa nchi zilizowekewa vikwazo; mkakati wa kuvifanya vikwazo kutokuwa na taathira
(last modified Tue, 14 Mar 2023 11:23:02 GMT )
Mar 14, 2023 11:23 UTC
  • Ushirikiano wa nchi zilizowekewa vikwazo; mkakati wa kuvifanya vikwazo kutokuwa na taathira

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria mambo mengi ya pamoja na yanayofanana yaliyopo kati ya Iran na Belarus na kueleza kuwa nchi zilizowekewa vikwazo na Marekani zinapasa kufanya kazi kwa pamoja ili kuondoa kizuizi hicho.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, amesema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo hapa Tehran na Rais wa Belarus Alexander Lukashenko na ujumbe aliofutana nao na akasema: Moja ya masuala yanayozikabili kwa pamoja Iran na Belarus ni vikwazo vya kibabe na kidhalimu vya Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi.

Ameongeza kuwa nchi ambazo zinakabiliwa na vikwazo vya Marekani zinapasa kushirikiana na kuunda taasisi ya pamoja na hivyo kuondoa kizuizi hicho na tunaamini kuwa hilo linawezekana."  

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran tokea mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kushtadi vikwazo hivyo katika miaka 12 iliyopita na kusema: Vikwazo vikali viliifanya Iran itambue uwezo na nguvu zake za ndani; na katika kipindi hicho cha kuwa chini ya vikwazo kumeandaliwa nyanja za maendeleo makubwa kwa ajili ya Iran na nchi yetu imeweza kufikia maendeleo makubwa katika nyanja mbalimbali ikiwemo za sayansi na teknolojia, matibabu na baolojia, teknolojia ya anga za mbali, nyuklia na nano." 

 

Vikwazo vimeendelea kufanywa kuwa moja ya wenzo wa madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani wa kuleta mashinikizo ya kiuchumi na kisiasa kwa mataifa yanayojitawala na yasiyokubali kuburuzwa. Lengo la vikwazo hivi vya kidhalimu ni kuyatenda mataifa lengwa na hivyo kuyafanya yasalimu amri na kubadilisha sera na misimamo yao.

Kiongozi Muadhamu katika mazungumzo na Rais wa Belarus (katikati), na Rais wa Iran, Sayyid brahim Raisi mjini Tehran 

 

Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana Marekani na washirika wake kwa miaka mingi sasa wamekuwa wakitumia wenzo wa vikwazo dhidi ya madola huru na ambayo yana ushindani nayo. Vikwazo hivyo vya kidhulma, vya upande mmoja na visivyo vya kisheria vimeziandama nchi kama Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Belarus, Russia, Syria, Venezuela na Cuba.

Hii ni katika hali ambayo, hegemonia (mamlaka ya kutoa amri) ya kisiasa na kiuchumi ya Magharibi imo katika hali ya kupungua na kudhoofika huku ulimwengu ukielekea upande wa kambi kadhaa. Mataifa yaliyowekewa vikwazo kama Iran, Russia na China hivi sasa yamo katika kuimarisha zaidi uhusiano na kupunguza kuegemea upande wa Magharibi na hata kuondokana kabisa na matumizi ya sarafu ya dola. Kuundwa miungano ya kieneo na kimataifa katika kalibu ya Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai au Jumuiya ya Brics ni hatua ambazo zinaweza kutathminiwa katika uwanja huu.

Marais wa Iran na Belarus wakibadilishana hati baada ya kutiliana saini makubaliano ya ushirikiano katika nyanja mbalimbali

 

Kwa muktadha huo, tajiriba na uzoefu wa mataifa yaliyowekewa vikwazo unaonyesha kuwa, sera za vikwazo hususan zinazotekelezwa na Marekani si kwamba, daima zina taathira. Hii ni kutokana na kuwa, uhalisia wa mambo ni kwamba, uchumi wa dunia umo katika hali ya kubadilika na wakati huo huo, ulimwengu unaelekea upande wa kambi kadhaa.

Katika mazingira haya inaonekana kuwa, kama mataifa yaliyowekewa vikwazo yatategemea nguvu zao na wakati huo huo kudumisha ushirikiano baina yao yataweza kupiga hatua kwa kasi kuelekea katika ustawi na maaendeleo. Mfano wa wazi ni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo licha ya kuandamwa na vikwazo na mashinikizo tangu kupatikana ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu lakini ikitegemea nguvu na wataalamu wa ndani imeweza kupiga hatua kubwa katika nyuga mbalimbali na kuchomoza na kuwa miongoni mwa mataifa ya mwanzo katika masuala mengi ya kielimu na kiteknolojia.

 

Hapana shaka kuwa, Belarus nayo kama ilivyo Iran inaandamwa na vikwazo vya Magharibi na kwa kuimarisha ushirikiano wake wa kiuchumi na Iran inaweza kulifanya hilo kama fursa ya kupunguza makali ya vikwazo.

Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana Rais wa Belarus akasema katika mazungumzo yake na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwamba, Iran imepata tajiriba na maendeleo makubwa katika kipindi cha vikwazo na tunaamini kuwa iwapo kipindi cha chini ya vikwazo kitatumiwa vyema inaweza kuwa fursa kwa ajili ya maendeleo.