Ripoti: Baadhi ya mashirika ajinabi yalihusika na mauaji ya polisi wa Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i95584-ripoti_baadhi_ya_mashirika_ajinabi_yalihusika_na_mauaji_ya_polisi_wa_iran
Baraza Kuu la Haki za Binadamu la Iran (HCHR) limechapisha ripoti mpya iliyofichua nafasi ya nchi za Magharibi na mashirika yao katika mauaji ya askari polisi wa Jamhuri ya Kiislamu wakati wa maandamano ya karibuni yaliyochochewa na mataifa hayo ya kibeberu hapa nchini.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 27, 2023 08:09 UTC
  • Ripoti: Baadhi ya mashirika ajinabi yalihusika na mauaji ya polisi wa Iran

Baraza Kuu la Haki za Binadamu la Iran (HCHR) limechapisha ripoti mpya iliyofichua nafasi ya nchi za Magharibi na mashirika yao katika mauaji ya askari polisi wa Jamhuri ya Kiislamu wakati wa maandamano ya karibuni yaliyochochewa na mataifa hayo ya kibeberu hapa nchini.

Ripoti hiyo ya kurasa 83 imeweka bayana namna mashirika ya Kimagharibi yalivyohusika na mauaji ya maafisa usalama wa Iran wakati wa maandamano hayo yaliyofanyika kwa kisingizio cha kifo cha mwanamke Muirani, Mahsa Amini.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa, nchi hizo za ajinabi zimekuwa zikitumia kila mbinu kuyumbisha uthabiti na usalama wa nchi tokea baada ya Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, kama vile kutumia makundi ya kigaidi.

Baraza Kuu la Haki za Binadamu la Iran limeashiria mauaji ya kigaidi ya Wairani zaidi ya 17,000 katika kipindi cha miongo minne iliyopita na kueleza kuwa, maadui wametumia mbinu zote kuvuruga uthabiti hapa nchini, kwa kuwa wanashindwa kuvumulia ustawi na maendeleo yanayofanywa na taifa hili.

Wamagharibi walivyochochea maandamano nchini kwa kisingizio cha kifo cha Mahsa Amini

Ripoti hiyo imebainisha kuwa, "Wananchi wa Iran walitoa kipaumbele kwa maslahi ya taifa, na hatimaye wakajitenga na wafanya ghasia, na kwa mara nyingine wakaibuka washindi na kuvuka salama mtihani huo."

Hivi karibuni, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Nasser Kan’ani alisema ingawa serikali za Magharibi zinadai kwamba hazikuwa zikifuatilia mabadiliko ya utawala nchini Iran, lakini alisisitiza kuwa Tehran haitasahau kamwe kuhusika kwao katika ghasia hizo.