Ripoti: Wanadiplomasia wakuu wa Iran na Saudia kukutana Beijing Alkhamisi
(last modified Wed, 05 Apr 2023 12:11:46 GMT )
Apr 05, 2023 12:11 UTC
  • Ripoti: Wanadiplomasia wakuu wa Iran na Saudia kukutana Beijing Alkhamisi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian na mwenzake wa Saudi Arabia, Mwanamfalme Faisal bin Farhan Al Saud, wanatazamiwa kukutana katika mji mkuu wa China, Beijing kesho Alkhamisi.

Kwa mujibu wa habari zilizotangazwa leo, mkutano huo ambao utakuwa wa kwanza wa aina yake katika kipindi cha zaidi ya miaka saba, unalenga kuendeleza mchakato wa makubaliano ya hivi karibuni kati ya Tehran na Riyadh ya kufufua uhusiano baina ya nchi mbili.

Mkutano huo wa kesho utafanyika kufuatia mawasiliano kwa njia ya siku yaliyofanywa mara matatu kati ya Amir-Abdollahian na Bin Farhan al-Saud, ambapo wawili hao walijadili hatua za baadaye kuhusu mapatano ya kihistoria yaliyofikiwa kwa usuluhishi wa China pamoja na makubaliano mengine ya pande mbili.

Beijing ilichaguliwa kama mahali pa mkutano ili kupanua nafasi na mchango wake chanya wa upatanishi wa kurejeshwa uhusiano kati ya Iran na Saudia na kuwezesha kuanzishwa mawasiliano baina ya mataifa hayo mawili yenye nguvu ya eneo la Asia Magharibi.

Wakati huo huo, Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tayari amekubali mwaliko kutoka kwa Mfalme wa Saudi Arabia Salman bin Abdulaziz Al Saud wa kutembelea Riyadh.

Baada ya siku kadhaa za mazungumzo makali yaliyoandaliwa na China, Iran na Saudi Arabia zilikubaliana Machi 10 kurejesha uhusiano wao wa kidiplomasia na kufungua tena balozi zao na ofisi za uwakilishi wa kidiplomasia baada ya miaka saba ya mfarakano.

Katika taarifa ya pamoja baada ya kusaini makubaliano hayo, Tehran na Riyadh zimesisitiza ulazima wa kuheshimu mamlaka ya kitaifa ya kila mmoja na kujiepusha na kuingilia masuala ya ndani ya kila mmoja wao.

Aidha, zimeafiki kutekeleza makubaliano ya ushirikiano wa kiusalama yaliyotiwa saini Aprili 2001 na makubaliano mengine yaliyofikiwa Mei 1998 ili kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, kibiashara, uwekezaji, kiufundi, kisayansi, kitamaduni, michezo na masuala ya vijana.../

 

 

Tags