Siasa za uhasama za Saudia dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i9604-siasa_za_uhasama_za_saudia_dhidi_ya_iran
Mwenendo usio wa mantiki unaoonyeshwa na utawala wa Aal Saudi katika matukio ya Mashariki ya Kati na kushupalia kwake siasa za kufurutu mpaka na za kuvuruga hali ya mambo kwa ajili ya kuimarisha nafasi ya utawala huo vimefanyiwa uchambuzi na ukosoaji na duru nyingi za habari na za kisiasa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 20, 2016 08:14 UTC
  • Siasa za uhasama za Saudia dhidi ya Iran

Mwenendo usio wa mantiki unaoonyeshwa na utawala wa Aal Saudi katika matukio ya Mashariki ya Kati na kushupalia kwake siasa za kufurutu mpaka na za kuvuruga hali ya mambo kwa ajili ya kuimarisha nafasi ya utawala huo vimefanyiwa uchambuzi na ukosoaji na duru nyingi za habari na za kisiasa.

Toleo la jana Jumapili la gazeti la Egypt Times linalochapishwa nchini Misri limechapisha makala kuzungumzia vitendo visivyo vya mantiki vya watawala wa Saudia na kuandika kuwa, tangu ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, nchi hii imekuwa imegeuka kuwa jinamizi kwa viongozi wa Saudia.

Katika sehemu moja ya makala hiyo imeelezwa kuwa, japokuwa mpangilio na mgawanyo wa madaraka baina ya wanamfalme ndani ya Saudia ni kwa maslahi ya Mfalme Salman na mwanawe Muhammad, lakini panga pangua 43 zilizofanywa katika vyeo vya kisiasa na vya utawala pamoja na uunganishaji wizara na taasisi kuu 13 ni fagio kubwa lililopita ndani ya utawala huo kwa madhumuni ya kumwandalia mazingira ya kutawala Muhammad bin Salman na hivyo kutobakisha chembe ya shaka kuwa lengo la hayo ni kumweka kando Muhammad bin Nayef, mrithi halisi wa ufalme wa nchi hiyo.

Kwa mtazamo wa gazeti hilo la Misri utawala wa Aal Saud hauandamwi na matatizo ya ndani tu ya kiusalama, kijamii na kiuchumi lakini katika upeo wa kieneo pia utawala huo unakabiliwa na changamoto za kila aina.

Kampeni za uwashaji moto wa vita zinazotekelezwa na matakfiri katika nchi za Syria na Iraq pamoja na vita dhidi ya Yemen vimeweka kwenye faili la utendaji uliofeli wa utawala wa Aal Saud rekodi ya umwagaji damu na utumiaji gharama kubwa mno za fedha, ambayo imeufedhehesha na kuuaibisha utawala huo.

Katika faili hilo, urafiki wa Saudia na utawala wa Kizayuni wa Israel ni nukta nyengine muhimu ya kuzingatiwa. Hivi karibuni viongozi wa utawala wa Kizayuni walikiri na kutangaza waziwazi kwamba baadhi ya nchi za Kiarabu zimebadilisha mtazamo wa uhusiano wao na Israel na kwamba Tel Aviv imeingia kwenye awamu ya kupata uungaji mkono wa Saudia.

Wakati akihutubia kongamano la Kizayuni la Herzliya, Herzi Halevi, mkuu wa Intelijinsia wa Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel alitamka kuwa mabadiliko hayo yanaafikiana na malengo ya utawala huo na kwamba Israel, ikiwa pamoja na Saudia inatoa mchango muhimu katika vita vya Syria na Yemen.

Kwa hakika inapasa tuseme kuwa ili kujivua na jinamizi la muqawama na la kupata nguvu nafasi ya kistratijia ya Iran baada ya kufikiwa makubaliano ya nyuklia, Wazayuni wanautumia utawala wa Aal Saud na vibaraka wake wa kitakfiri kama vikosi vyake vya nchi kavu vya kudhamini usalama wake. Kupitia siasa hiyo utawala wa Kizayuni unayatumia makosa ya kistratijia yanayofanywa na Wasaudi ili kuzipotosha fikra za wananchi wa mataifa ya eneo zishughulike na adui bandia na wa kubuni na kumwacha adui yao halisi ambaye ni utawala huo ghasibu.

Saudia, ilitumia huko nyuma mabilioni ya dola kumsaidia Saddam katika vita dhidi ya Iran, ikawatumia pia magaidi wa kitakfiri kushambulia vituo vya kidiplomasia vya Iran katika nchi kadhaa na kuyatumia pia makundi ya kigaidi ili kuvuruga amani na uthabiti ndani ya Iran.

Utawala wa Saudia umehiyari hata kuuza mafuta yake kiholela kwa bei nafuu na kuutia msukosuko mkubwa uchumi wake kwa matumaini tu kwamba kwa kuyauza mafuta yake kwa bei ya che utaweza kuvuruga soko la mafuta na kupunguza pato linalotokana na mafuta la Iran.

Kwa hatua zake hizo Saudia imedhihirisha tu sura yake halisi katika eneo na ulimwengu mzima kuwa ni utawala wa shari, mvuruga amani, mwagaji damu na muungaji mkono wa ugaidi.

Na hii ni katika hali ambayo viongozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wanazitumia dola za Saudia na ugaidi wa kitakfiri unaoungwa mkono na utawala wa Riyadh ili kujidhaminia usalama wake. Sambamba na hayo, Marekani na Ulaya nazo zinafikiria kuiuzia Saudia silaha zenye thamani ya mabilioni ya dola na kuielekeza nchi hiyo kwenye siasa na sera za kuzusha mgawanyiko katika Mashariki ya Kati ili kuhalalisha uingiliaji wao katika eneo hili.

Uanzishaji muungano wa kimaonyesho wa kupambana na ugaidi chini ya uongozi wa utawala wa Aal Saud nao pia umefanywa kwa lengo la kufifisha ukweli kuhusu uungaji mkono ugaidi unaofanywa na utawala huo. Kashfa ya kuhusika raia 15 wa Saudia katika tukio la Septemba 11 na utoaji hongo ya dola bilioni 750 ili kuzuia kutolewa nyaraka za kashfa hiyo, yote hayo yanaweka wazi utambulisho na sura halisi ya Saudia. Lakini ajabu ya yote ni kwamba utawala wa Riyadh unaendelea kukariri madai yake hewa ya kuituhumu Iran kuwa eti inaunga mkono ugaidi na kuingilia masuala ya ndani ya nchi za eneo hili.../