Ujumbe wa Iran uko Saudi Arabia kuandaa ufunguzi wa ubalozi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i96200-ujumbe_wa_iran_uko_saudi_arabia_kuandaa_ufunguzi_wa_ubalozi
Ujumbe wa Iran umewasili katika mji mkuu wa Saudi Arabua, Riyadh, kujadili utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya pande hizo mbili mwezi uliopita ili kurejesha uhusiano wa kidiplomasia.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Apr 12, 2023 22:53 UTC
  • Ujumbe wa Iran uko Saudi Arabia kuandaa ufunguzi wa ubalozi

Ujumbe wa Iran umewasili katika mji mkuu wa Saudi Arabua, Riyadh, kujadili utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya pande hizo mbili mwezi uliopita ili kurejesha uhusiano wa kidiplomasia.

Katika taarifa yake, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Nasser Kan’ani, amesema "ujumbe wa kiufundi" kutoka Iran uliwasili Riyadh Jumatano na jana, na kukaribishwa na maafisa wa Saudia.

Amesema ujumbe wa Iran utachukua hatua zinazohitajika kufungua tena ubalozi mjini Riyadh na ubalozi mdogo mjini Jeddah, na pia mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) katika mji wa Jeddah.

Aliongeza kwamba, juhudi zitafanywa ili kufungua tena ofisi za uwakilishi wa Iran nchini Saudia kabla ya kuanza ibada ya Hija mwaka huu.

Kan’ani pia alisema kuwa ujumbe wa kiufundi wa Saudi Arabia, ambao ulikuwa umewasili Iran siku ya Jumamosi, leo Alhamisi utaelekea katika mji mtakatifu Mash'had kaskazini mwa Iran kwa lengo la kuandaa mazingira ya kufunguliwa tena ubalozi mdogo wa Saudia mjini humo.

Hatua hiyo inafuatia mkutano wa wiki iliyopita mjini Beijing kati ya mawaziri wa mambo ya nje wa Iran na Saudia, ambao walisisitiza haja ya kutekeleza makubaliano ya nchi mbili ili kuimarisha hali ya kuaminiana na kusaidia kuimarisha usalama katika eneo la Magharibi mwa Asia.

 Shamkhani, Musaid Al Aiban (kushoto), Waziri wa Nchi na mjumbe wa Baraza la Mawaziri wa Saudi Arabia ambaye pia ni  Mshauri wa Usalama wa Taifa, Wang Yi Mkurugenzi wa Ofisi ya Kamisheni Kuu ya Mambo ya Nje ya Chama cha Kikomunisti cha China Katibu wa Baraza Kuu la Usalama la Taifa la Iran (SNSC) Ali Shamkhani 

Huo ulikuwa mkutano wa kwanza rasmi wa mawaziri wa mambo ya nje wa Iran na Saudia baada ya zaidi ya miaka saba. Mnamo Machi 10, baada ya siku kadhaa za mazungumzo mazito yaliyoandaliwa na China, Iran, na Saudi Arabia zilikubali kurejesha uhusiano wao wa kidiplomasia na kufungua tena balozi zao.

Katika taarifa ya pamoja baada ya kusaini makubaliano hayo, Tehran na Riyadh zilisisitiza haja ya kuheshimu mamlaka ya kitaifa ya kila mmoja na kujiepusha na kuingilia masuala ya ndani ya kila mmoja wao.

Aidha pande mbili ziliafiki kutekeleza makubaliano ya ushirikiano wa kiusalama yaliyotiwa saini Aprili 2001 na makubaliano mengine yaliyofikiwa Mei 1998 ili kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, kibiashara, uwekezaji, kiufundi, kisayansi, kitamaduni, michezo na masuala ya vijana.

Mapatano hayo ya Iran na Saudia, ambayo yamezikera sana Marekani na Israel, yanaweza kupunguza mivutano katika eneo la Asia Magharibi ambalo limekumbwa na machafuko kwa miongo kadhaa.