Iran na Saudia zimo kwenye mkondo wa kuimarisha uhusiano wa kiuchumi
Waziri wa Uchumi wa Iran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu na Saudi Arabia hivi sasa zimo kwenye mkondo wa kuimarisha uhusiano wao wa kiuchumi na wameshafikia hatua nzuri.
Kwa mujibu wa shirika la habari la ISNA, Sayyid Ehsan Khandozi ambaye siku ya Alkhamisi alikuweko mjini Jeddah Saudi Arabia kushiriki katika kikao cha kila mwaka cha Benki ya Maendeleo ya Kiislamu (IsDB) jana alionanaa na waziri mwenzake wa uchumi wa Saudia pembeni mwa kikao hicho. Amesema katika mahojiano aliyofanyiwa na gazeti la al Sharq al Awsat kwamba, ana imani Iran na Saudia zitafanikiwa katika mkondo wa kuimarisha uhusiano na ushirikiano wao wa kiuchumi.
Amesema, siasa kuu za serikali mpya ya Iran ni kuimarisha uhusiano wake na majirani zake zikiwemo nchi za Kiarabu na kufafanua zaidi kwa kusema: Iran inakaribisha juhudi zozote za kukurubisha zaidi uhusiano wake na majirani zake zikiwemo nchi za Kiarabu na kuwa na uhusiano bora kabisa na nchi hizo.
Waziri wa Uchumi wa Iran vile vile amesema, ajenda ya serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na mapendekezo yetu ni kuhakikisha kunafanyika jitihada kubwa za kuweza kuishinda migogoro wa kiuchumi, kubadilishana teknolojia baina ya nchi za Waislamu na kupanua mno wigo wa ushirikiano wa kiuchumi baina ya nchi za dunia, hususan za ukanda huu.
Kikao cha kila mwaka cha Benki ya Ustawi wa Kiislamu kilianza rasmi jana Ijumaa mjini Jeddah Saudi Arabia kwa kuhudhuriwa na viongozi kutoka zaidi ya nchi 50 duniani, wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, OIC.