Raisi: Umoja na mshikamano wa Waislamu ni jambo muhimu, la kimkakati
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameutaja mshikamano, umoja na mfungamano wa Waislamu kuwa ni jambo muhimu na la kistratijia.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Iran, mwishoni mwa ziara yake rasmi ya siku mbili nchini Indonesia, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Sayyid Ebrahim Raisi, jana Jumatano, alihudhuria katika Msikiti wa Istiqlal nchini humo, kwa ajili ya Swala ya Adhuhuri, na akaeleza kufurahishwa kwake kutokana na kushirikiana na wananchi wa Indonesia katika ibada hiyo.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameutaja mshikamano, umoja na mfungamano wa Waislamu kuwa ni jambo muhimu sana na la kistratijia na akasema: Umoja na mshikamano huu haupaswi kamwe kusahauliwa kwa sababu ni mji mtaji mkubwa wa Indonesia na Ulimwengu wa Kiislamu. Amesema, mbali ya kuwa ni sehemu ya mikusanyiko na ibada, misikiti inapaswa pia kuwa dhihirisho la majukumu ya kijamii ya Waislamu.
Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu amekutaja kuwajali wanadamu wengine katika kalinu ya kumwamini ipasavyo Mwenyezi Mungu kuwa ni miongoni mwa mambo muhimu yanayopaswa kushughulikiwa na misikiti na akaongeza kuwa: Leo hii ni jukumu la Waislamu kujali na kutilia maanani haki za wananchi wa Palestina wanaoteseka kutokana na dhulma za mabeberu, na pia kuipa mazingatio hali ya watu wa Myanmar na sehemu nyingine za dunia ambao wanasumbuliwa na matatizo. Amesisitiza kuwa kuyajali mambo haya kunamfanya mjaa apate radhi za Mwenyezi Mungu.
Rais Ebrahim Raisi amesema adui anaeneza chuki na propaganda chafu dhidi ya Uislamu duniani na vilevile chuki dhidi ya Iran (Iranophobia) miongoni mwa Waislamu. Amesema: Waislamu duniani wanajua kwamba rafiki yao bora anayejali utu na uhuru wao, na anayelinda heshima zao, ambaye anautambua ukosefu wa usalama wa Waislamu wengine kuwa ni ukosefu wa usalama wake yeye mwenyewe, ni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.